TANZANIA-HAKI-USHOGA

Gavana wa Dar es Salaam atoa wito wa kuwafichua mashoga nchini Tanzania

Mji wa Dar es-Salaam Tanzania.
Mji wa Dar es-Salaam Tanzania. Wikimédia/Muhammad Mahdi Karim

Gavana wa mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda amezindua kampeni dhidi ya ushoga, akitoa wito kwa wananchi wake kuwafichua mashoga, huku akiahidi kuwa operesheni ya kuwakamata itaanza wiki ijayo.

Matangazo ya kibiashara

"Nina taarifa za kuwepo kwa mashoga wengi katika mkoa wetu," ambao ni pamoja na mji wa Dar es Salaam, mji mkuu wa kiuchumi wa nchi hii, amesema Paul Makonda katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu jioni.

"Mashoga hawa wamekuwa wakijisifu kwenye mitandao ya kijamii. Kuanzia leo (Jumatatu) mpaka Jumapili, nawaomba mnipe majina yao," Paul makonda amewaomba viongozi tawala katika mkoa wa dar es Salaam.

"Timu itaanza operesheni ya kuwakamata siku ya Jumatatu ya wiki ijayo," ameahidi Paul Makonda, afisa wa chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM), na mshirika wa karibu na Rais John Pombe Magufuli, ambaye pia anapinga ushoga.

"Najua kwamba ninapokemea ushoga, kuna nchi ambazo zinaniona adui. Lakini mimi naona afadhali nikasirisha nchi hizo kuliko kumkosea Mungu," ameongeza Bw Makonda.

Gavana Makonda, mwenye imani ya Kikristo, amewataka wananchi wenzake kuunga mkono kampeni yake dhidi ya ushoga, ambao, amesema, "umepoteza maadili ya Watanzania na dini zetu zote mbili Ukristo na Uislamu."

Ushoga ni uhalifu nchini Tanzania, unaoadhibiwa kwa kifungo cha chini cha miaka 30 hadi kifungo cha maisha. Jamii ya Watanzania haiungi mkono ushoga, kitendo kinachofanyika kwa siri.