SUDANI KUSINI-MACHAR-SIASA-USALAMA

Riek Machar arejea Juba, Sudan Kusini

Kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini Riek Machar, hapa ilikuwa Februari 2014. du Sud.
Kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini Riek Machar, hapa ilikuwa Februari 2014. du Sud. REUTERS/Goran Tomasevic

Kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini, Riek Machar, yuko mjini Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini tangu mapema asubuhi katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba,  baada ya miaka miwili akiwa uhamishoni.

Matangazo ya kibiashara

Riek Machar alishiriki katika sherehe ya kutiliwa saini ya mkataba wa amani mwezi Septemba, licha ya wasiwasi kuhusu usalama wake, mmoja wa wasemaji wake ametangaza.

Bw Machar, kiongozi wa kundi la waasi la SPLM-IO, "atasafiri kwenda Juba kwa sherehe ya amani" , amesema mmoja wa wasemaji wake, Lam Paul Gabriel.

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir, hasimu mkuu wa Machar, na marais kadhaa wa ukanda huo wamehudhuria sherehe hiyo ambayo ilifanyika katika kuadhimisha mkataba wa amani wa Septemba 12 uliotiliwa saini mjini Addis Ababa, nchini Ethiopia. Mkataba ambao unasitisha miaka mitano ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Bw Machar, ambaye chini ya mkataba huo anatarajia kushikilia nafasi yake ya zamani kama makamu wa rais, hajarudi Juba tangu alipokimbia mji mkuu mwezi Julai 2016 baada ya mapigano yaliyosababisha vifo vingi kati ya wapiganaji wake na majeshi ya serikali.

Riek Machar ambaye alitoroka nchi hiyo tangu wakati huo, baada ya kukimbia kwa miguu na askari wake wakipitia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) "anahofia usalama wake," amekiri msemaji wake.

"Lakini ukweli upo: sisi ni watu wa amani na hicho ndicho tunajaribu kufanya, kuleta uaminifu kwa wananchi," amesema Lam Paul Gabriel, akiongeza kuwa Bw Machar atasafiri na wanasiasa thelathini wa SPLM-IO, bila ya kusindikizwa na askari.

Mnamo mwezi Aprili 2016, Bw Machar alikuwa tayari kurudi Juba ili aendelee na majukumu yake kama makamu wa rais chini ya mkataba wa amani uliofikiwa Agosti 2015. Kurudi kwake kulikuwa kuzua mjadala mkubwa kuhusu idadi na vifaa vya askari ambao wangeliweza kuongozana naye.

Wadadisi wanasema kuwa ushirikiano kati ya Salva Kiir na riek Machar hautazaa matunda yoyote, ikilinganishwa na hali iiyotokea awali.

Miaka miwili na nusu baada ya uhuru, Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo mwezi Disemba 2013 huko Juba, wakati Bw Kiir, kutoka kabila la Dinka, alimshtumu Bw Machar, Makamu wa zamani wa rais, kutoka kabila la Nuer, kupanga jaribio la mapinduzi.

Machafuko hayo yaliyochochewa kikabila yalisababisha watu zaidi ya 380,000 kupoteza maisha, kulingana na uchunguzi wa hivi karibuni, na kusababisha watu zaidi ya milioni nne, karibu theluthi moja ya idadi ya watu wa Sudan Kusini, kutoroka makazi yao.