BURUNDI-AU-MAZUNGUMZO-SIASA-USALAMA

Umoja wa Afrika kutafutia ufumbuzi mgogoro wa Burundi

Benjamin Mkapa, Mratibu wa mazungumzo ya amani kuhusu Burundi.
Benjamin Mkapa, Mratibu wa mazungumzo ya amani kuhusu Burundi. EBRAHIM HAMID / AFP

Baada ya kumalizika kwa awamu ya tano ya mazungumzo ya warundi mapema juma hili huko mjini Arusha nchini Tanzania, na kususiwa na serikali na washirika wake, kuna uwezekano Umoja wa Afrika kushughulikia mgogoro unaoikabili nchi ya Burundi.

Matangazo ya kibiashara

Ni swali ambalo wengi wangelipenda kufahamu baada ya kushindwa kupatikana kwa suluhu ya mgogoro wa Burundi hasa kutokana na serikali pamoja na washirika wake kususia vikao hivyo.

Muwezeshaji katika mgogoro huo Benjamin William Mkapa sasa anarudisha jukumu kwa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki waliomteuwa ambao hata hivyo wanatuhumiwa kutompa ushirikiano wa kutosha.

Baada ya kuongoza usuluhishi kwa kipindi cha miaka 3 kilichoanza mwaka 2015 baada ya rais Pierre Nkurunziza kutangaza kuwania muhula wa 3, miezi kadhaa baadae Benjamin Mkapa aliepewa jukumu la kuratibu mazungumzo na ambapo Jumatatu ndipo alitangaza kufikia tamati ya jukumu lake.

Katika ukumbi wa mikutano, wanasiasa wa upinzani walioitoroka Burundi pamoja na wale waishio nchini Burundi walionyesha kutoridhishwa na kufeli kwa mazungumzo hayo na hasa namna viongozi wa Jumuiya ya Afrika mashariki wanavyouchukulia mzozo wa Burundi.

Rasmi ni kwamba rais wa zamani wa Tanzania anaandaa ripoti ambayo atawasilisha kwa msuluhishi rais wa Uganda yoweri Museveni na baadae ndipo viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ndio wataoamuwa nini kitachofuata. Lakini hata hivyo Umoja wa Afrika ambao ndio ulioipa jukumu la usuluhishi Jumuiya ya Afrika mashariki na ambao ulitishia kuingilia kati iwapo mazungumzo hayo yatafeli, huenda ukachukuwa jukumu lake, wakati huu serikali ya Bujumbura ikiendelea kuandaa taratibu za uchaguzi wa mwaka 2020 huku ukisisitiza kuwa kila kitu kinakwenda sawa.