TANZANIA-AMNESTY-HAKI-USHOGA

Tanzania: Hatua za Paul Makonda dhidi ya mashoga ni mawazo yake binafsi

Mji wa Dar es-Salaam, Tanzania.
Mji wa Dar es-Salaam, Tanzania. Wikimédia/Muhammad Mahdi Karim

Serikali ya Tanzania imejiweka kando na hatua za hivi karibuni zilizotangazwa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye alitangaza operesheni ya kuwakamata watu wanaotuhumiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Matangazo ya kibiashara

Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumapili na wizara ya mambo ya nje ya Tanzania, imesema kuwa hatua zilizotangazwa kuchukuliwa na Paul Makonda ni mawazo yake binafsi na sio msimamo wa Serikali ya Tanzania.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuheshimu mikataba yote ya kimataifa inayohusu haki za binadamu ambayo imesaini na kuridhia.

Kauli ya wizara ya mambo ya nje imetolewa juma moja tu tangu mkuu wa mkoa huyo wa mkoa wa Dar es salaam, atoe wito kwa wananchi kumtumia majina ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia, tangazo ambalo limeibua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii.

Tayari mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yameonesha kuguswa na tangazo hili na kuonya dhidi ya uwezekano wa kudhuriwa kwa watu waliotajwa kujihusisha na ushoga.

Wakati huo huo Shirika la kimataifa la Haki za Binadaamu la Amnesty International limelelezea wasiwasi wake kufuatia hatua ya Gavana wa mkowa wa Dar es Salaam Paul Makonda ya kuwataka wakazi wa mkoa huo kuwafichua watu wa mapenzi ya jinia moja (mashoga).

Amnesty International inasema kuwa hatua ya kuwakamata na kuwashikilia watu kutoka jamii hiyo inaendeshwa kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.