TANZANIA-KASSIM MAJALIWA-KOROSHO

Serikali ya Tanzania kuwafutia leseni wafanyabiashara watakaoshindwa kununua zao la Korosho

Serikali ya Tanzania imewataka wanunuzi wa zao la korosho kutaja tani watakazonunua katika kipindi cha siku nne. 

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa Mwananchi
Matangazo ya kibiashara

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ametolewa kauli hiyo leo wakati akizungumza kupitia Televisheni ya Taifa, TBC akiwa Ofisini kwake Mlimwa Mkoani Dodoma.

Majaliwa amesema baada ya siku nne kupita, serikali italazimika kufuta usajili wa wale wote waliojisajili kununua zao hilo.

"Mwenye nia ahakikishe anafanya hivyo katika siku nne, serikali italazimika kufuta usajili wa kununua zao hilo. Wafanyabiashara wana nafasi ya kuleta wakati wowote wakionesha nia na kiwango wanchotaka, zaidi ya hapo serikali haitaruhusu kampuni yoyote kununua korosho tena,"amesema Mtendaji huyo Mkuu wa Serikali ya Tanzania.

Zao la Korosho hulimwa kwa wingi na wananchi wa mikoa ya Kusini mwa Tanzania, Lindi na Mtwara na ni tegemeo lao kubwa kiuchumi.

Awali wakulima wa zao hilo waligoma kuuza wakilalamikia bei ndogo ikilinganishwa na ya msimu uliopita, hatua iliyosababisha serikali kuingilia kati na kuwashawishi wafanyabiashara kununua kwa bei isiyopungua Shilingi 3000 ya Tanzania kwa kilo.