BURUNDI-SIASA-USALAMA

Askari watatu wa Burundi wakamatwa katika kambi ya wakimbizi DRC

Kambi ya wakimbi wa Burundi ya Lusenda, mashariki mwa DRC.
Kambi ya wakimbi wa Burundi ya Lusenda, mashariki mwa DRC. Sébastien Bonijol

Watu watatu wanaoshukiwa kuwa askari wa Burundi wamekamatwa baada ya kuingia kinyume cha sheria katika kambi ya wakimbizi kutoka Burundi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Matangazo ya kibiashara

"Watu watatu waliokuwa na vibali vya jeshi la Burundi wamekamatwa katika kambi ya wakimbizi wa Burundi ya Lusenda ambapo waliingia kinyume cha sheria," chanzo cha kijeshi ambacho hakikutaja jina kililiambia shirika la Habari la AFP.

"Watu watatu wanaoshukiwa kuwa raia wa Burundi ambao waliingia kinyume cha sheria nchini DRC wamekamatwa na jeshi la FARDC katika kambi ya wakimbizi ya Lusenda," amesema kwa upande wake Kapteni Dieu-Donné Kasereka, msemaji wa jeshi la DRC katika mkoa wa Kivu Kusini. "Kwa sasa watu hawo wanahojiwa na kitengo cha idara ya ujasusi katika jeshi la DRC," afisa huyo ameongeza, huku akikakataa kusema kama ni askari wa jeshi la Burundi.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya kijeshi nchini DRC, hivi karibuni kulitokea mapigano kati ya waasi wa Burundi wa Red-Tabara na jeshi la Burundi katika milima ya Sange karibu na mpaka wa Burundi baada ya askari kadhaa wa jeshi hilo kuingia nchini DRC.

Kwa mujibu wa mashahidi askari wengi wa Burundi waliuawa katika mapigano hayo na wengine kulazimika kujificha katika nyumbani za wakazi wa Sange na maeneo jirani, kutokana na kwamba walikuwa hawafahamu maeneo hayo.

Lakini jeshi la Burundi limekanusha madai hayo na kusema hakuna askari wa Burundi aliingia nchini DRC.

Katikati mwa mwezi Septemba 2017, wakimbizi 34 waliuawa katika kambi hii ya Lusenda baada ya kuzuka makabiliano na askari wa DRC.

Burundi inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa tangu Rais Pierre Nkurunziza kuwania katika uchaguzi wa urais kwa muhula wa tatu na kupelekea ushindi wake mnamo mwezi Julai mwaka huo huo. Uchaguzi ambao ulisusiwa na upinzani.

Machafuko nchini Burundi yamesababisha watu kati ya 500 na 2,000 kupoteza maisha, kwa mujibu wa vyanzo vya Umoja ww Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali), mamia ya watu wametoweka, huku zaidi ya watu 400,000 wakilazimika kuyahama makazi yao.

Zaidi ya wakimbizi 36,000 wanapewa hifadhi nchini DRC, ambako wanaishi katika kambi ya Lusenda na makambi mengine mashariki mwa nchi hiyo.