DRC-UGANDA-ZIWA ALBERT

Wavuvi saba wauawa katika Ziwa Albert nchini Uganda

Ziwa Albert ambalo linalounganisha nchi za DRC na Uganda
Ziwa Albert ambalo linalounganisha nchi za DRC na Uganda DISPATCH.UG

Watu wenye silaha, wanaoshukiwa kuwa waasi kutoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wameuwa wavuvi saba raia wa Uganda katika Ziwa Albert.

Matangazo ya kibiashara

Mauaji haya yamethibitishwa na Naibu Kamanda wa jeshi la Polisi kayika Wilaya ya Hoima Amos Muhindo.

Muhindo anasema watu hao wenye silaha, waliwafatulia risasi wavuvi hao, wakati wakiwa katika harakati za kuutafuta mwili wa mwezao aliyekuwa amezama katika Ziwa hilo.

Aidha, amesema ni mtu mmoja tu ndiye aliyeponea shambulizi hilo,na anaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Hoima.

Inaelezwa kuwa, watu hao walikuwa watano, na walikuwa wamevalia mavazi ya jeshi. Hii ni mara ya tatu kwa kipindi cha wiki moja, ambapo wenye silaha wameshambulia wavuvi wa Uganda.

Kumekuwa na hali ya wasiwasi kati ya serikali ya Kinshasa na Kampala kuhusu wavuvi kuuawa katika Ziwa Albert, huku kila upande ukisema wavuvi wa pande zote mbili wanavuka mpaka na kuvua katika eneo ambalo sio lake.

Mwezi Julai, wanajeshi wa DRC na Uganda walikabiliana katika Ziwa hilo na kusababisha maafa.