TANZANIA-UHURU WA KUJIELEZA-HAKI

Mwaka mmoja tangu kutoweka kwa Azory Gwanda, maswali ni mengi kuliko majibu

Mwanahabari wa gazeti la Mwananchi Azory Gwanda alitoweka Novemba 21, 2018
Mwanahabari wa gazeti la Mwananchi Azory Gwanda alitoweka Novemba 21, 2018 Daily Nation

Siku, miezi na hatimaye mwaka mmoja umetimia tangu mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda alipotoweka katika eneo la Kibiti Mkoani Pwani.

Matangazo ya kibiashara

Maswali yanayosalia katika kipindi cha siku zaidi ya 360 ni moja nalo ni wapi alipo mwanahabari huyo na ikiwa yu hai au ameuawa na watesi wake wana shabaha ipi.

Gwanda alikuwa akiandikia gazeti la Mwananchi na alitekwa Novemba 21 mwaka 2017 akiwa katika eneo la Kibiti Mkoani, Pwani.

Tangu kutekwa kwake, vyombo vya habari vya ndani na nje ya Tanzania vimeripoti kwa kina tukio hilo huku pia wanaharakati wa haki za binadamu nchini Tanzania wakipaza sauti wakitaka uchunguzi ufanywe kuhusu kutoweka kwa mwanahabari huyo.

Hata hivyo, serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Mambo ya ndani, Kangi Lugola imekuwa ikisisitiza kwamba inafanya uchunguzi wa visa vyote vya kutoweka kwa watu wakiwemo wanahabari, kupitia Jeshi la Polisi.

RFI imezungumza na waandishi wa Mwananchi ambao wanasema tukio la kutekwa kwa Azory limeongeza hofu hususani kwa waandishi wanaofanya habari za uchunguzi.

"Tukio hili linaongeza hofu kwa wanahabari hasa wanaofanya habari za uchunguzi,"amesema Benard James, mhariri katika gazeti hilo.

Tangu kutoweka kwa mwanahabari huyo, taasisi za kihabari za ndani na nje ya Tanzania, ikiwemo Shirika la Wanahabari wasiokuwa na Mipaka (RSF) yamepaza sauti kutaka mamlaka za Tanzania kuchunguza kisa cha kutoweka kwa mwanahabari huyo.

Sikiliza Ripoti kuhusu mwaka mmoja tangu kutekwa kwa Azory Gwanda kupitia kiunganishi hapo juu