KENYA-UGAIDI-AL SHABAB-SOMALIA

Washukiwa wa Al Shabab wamteka raia wa Italia na kuwajeruhi watano, Pwani ya Kenya

Barabara katika kijiji cha Chakama
Barabara katika kijiji cha Chakama dailyactive

Watu wenye silaha wamemteka raia wa Italia, katika kijiji cha Chakama, katika kaunti ya Kilifi Pwani ya Kenya.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti zinasema kuwa, watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Al Shabab ndio waliohusika.

Imebainika kuwa raia huyo wa kigeni, mwenye umri wa miaka 23 ambaye pia mfanyikazi wa kujitolea na watu wengine watano, walijeruhiwa katika makabiliano yaliyoshuhudiwa.

Polisi wanasema mtoto mwenye umri wa miaka 10, ni miongoni mwa watu hao waliojeruhiwa. Imeelezwa kuwa, mtoto huyo alipigwa risasi machoni na anaendelea kupata matibabu hospitalini.

Utekaji nyara nchini Kenya sio jambo la kawaida, lakini linapotokea, limekuwa likisababisha madhara kwa sekta ya utalii nchini humo.

Mwaka 2011, raia wa Uingereza aliuawa kwa kupigwa risasi na mkewe akatekwa huku Mwanamke mmoja raia wa Ufaransa akitekwa na watu wenye silaha nyumbani kwake katika kisiwa cha Lamu.

Aidha, wafanyikazi wawili wa Shirika la kutoa msaada kutoka nchini Uhispania pia walitekwa.

Kundi la Al Shabab lenye makao yake nchini Somalia, limekuwa likivuka mpaka na kuingia nchini humo na kutekeleza utekaji huo.

Hii ndio iliyokuwa sababu kubwa ya serikali ya Kenya kuamua kuwatuma wanajeshi wake nchini Somalia.