BURUNDI-MELCHIOR NDADAYE-MAUAJI-SIASA

Wanajeshi wanne wa zamani wakamatwa kwa madai ya kuhusika na kifo cha Melchior Ndadaye

Melchior Ndadaye, rais wa zamani wa Burundi.
Melchior Ndadaye, rais wa zamani wa Burundi. © AFP/DABROWSKI

Serikali nchini Burundi inasema, wanajeshi wanne wa zamani wamekamatwa wakihusishwa na mauaji ya aliyekuwa rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia, Melchior Ndadaye aliyeuawa mwaka 1993.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa mashtaka Sylvestre Nyandwi amesema, ofisi yake ina ushahidi kuwa wanne hao walihusika, kwa kupanga na kutekeleza mauaji hayo.

Hata hivyo, hakutaja majina ya washukiwa hao lakini akaongeza kuwa washukiwa wengine watakamatwa na kufikishwa Mahakamani.

“Tulichukua muda wetu kukusanya ushahidi na kesi hii ya mauaji bado ipo katika Mahakama ya Juu, na tunafanya hivi ili kutoficha uovu katika nchi yetu,” alisema Nyandwi.

Ndadaye, alitoka kabila la Mhutu na aliuawa miezi mitatu baada ya kuchaguliwa, Oktoba 21 mwaka 1993.

Mauaji yake, yalisababisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo yaliyodumu kwa zaidi ya miaka 10 na kusababisha vifo vya watu 300,000.

Raia wa Burundi, wanaamini kuwa Ndadaye ndio shujaa wa demokrasia na siasa nchini humo, aliyeanzisha chama cha FRODEBU.