RWANDA-SIASA-USALAMA-HAKI

Rwanda yamshikilia mwandishi wa habari wa kujitegemea kwa madai ya ugaidi

Polisi nchini Rwanda kitengo cha upelelezi inamshikilia mwandishi wa habari wa kujitegemea Phocus Ndayizera aliyeripotiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha juma lililopita.

Mji wa Kigali, ambako mwandishi wa habari wa kujitegemea Phocus Ndayizera anazuliwa.
Mji wa Kigali, ambako mwandishi wa habari wa kujitegemea Phocus Ndayizera anazuliwa. Getty/Peter Stuckings
Matangazo ya kibiashara

Phocus Ndayizera ambaye alifanyia kazi vyombo vya habari mbali mbali ameonyeshwa mbele ya vyombo vya habari na polisi wa upelelezi nchini Rwanda wiki moja baada yake kutoweka.

Bw Ndayizera mara kwa mara amekuwa akiripotia BBC Idhaa ya Kinyarwanda na Kirundi.

Mara baada ya kuoneshwa mbele ya waandishi wa habari, idara ya upelelezi imedai amekamatwa na vitu vinavyodhaniwa ni mabomu ambavyo alitaka kuvilipua katika maeneo mbalimbali ya taifa la Rwanda. Tuhuma ambazo Mwanahabari huyo ametuppilia mbali. 

Mwandishi huyo anayeishi wilayani Muhanga kusini mwa Rwanda alioneshwa siku ya Jumatano katika makao makuu ya idara ya upelelezi yaliyopo Kacyiru jijini Kigali.

Msemaji wa RIB, Modeste Mbabazi, ameviambia vyombo vya habari kuwa, Phocus alikamatwa maeneo ya Nyamirambo muda mfupi mara baada ya kukabidhiwa mabomu hayo wiki iliyopita.