KENYA-UGAIDI-SOMALIA

Kenyatta: Tumepoteza wakenya 14, magaidi wameuawa na operesheni imekamilika

Maafisa wa usalama wakiwasaidia watu kutoroka kwenye hoteli ya Dusit jijini Nairobi Januari 15 2019
Maafisa wa usalama wakiwasaidia watu kutoroka kwenye hoteli ya Dusit jijini Nairobi Januari 15 2019 Photo: Kabir Dhanji/AFP

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametangaza kuwa magaidi wote walioshambulia hoteli ya kifahari ya Dusit wameuawa na operesheni ya kuwaokoa watu waliokuwa wamekwama katika majengo ya eneo hilo Magharibi mwa jiji kuu la Nairobi, imemalizika baada ya saa 20.

Matangazo ya kibiashara

“Nathibitisha kuwa, operesheni za kiusalama katika eneo la Dusit limekamilika na magaidi wote wameuawa,” amesema rais Kenyatta akilihotubia taifa Jumatano asubuhi.

Watu waliopoteza maisha katika tukio hili ni 14 lakini idadi ya wengine isiyojulikana wamejeruhiwa.

“Kwa sasa tunathibitisha kuwa watu waliopoteza maisha mikononi mwa magaidi ni 14, lakini wengine wamejeruhiwa,” aliongeza rais Kenyatta.

Aidha, amesema kuwa maafisa wa polisi na wasamaria wema walifanikiwa kuwaokoa watu 700.

Hata hivyo, haijafahamika magaidi waliotekeleza shambulizi hilo walikuwa wangapi lakini kamera za cctv zimeonesha watu wanne wakiwa na silaha wakiingia katika eneo la hoteli hiyo.

Polisi wamethibitisha kuwa, washambuliaji wawili waliuawa katika makabiliano makali ya risasi.

Rais Kenyatta, amewataka wakenya kurejea kazini huku akisema kuwa Kenya haisahau wale wote wanaowaumiza watoto wa nchi hiyo.

“Nchi iko salama, na hatutatishwa na tukio hili,” amesema rais Kenyatta.