KENYA-USALAMA-UGAIDI

Kenya: Watuhumiwa wakamatwa baada ya shambulio dhidi ya hoteli ya kifahari

Maafisa wa uchunguzi wakiwa mbele ya hoteli ya kifahari ya DusitD2 iliyolengwa na shambulizi la kigaidi, Nairobi, Kenya, Januari 17, 2019.
Maafisa wa uchunguzi wakiwa mbele ya hoteli ya kifahari ya DusitD2 iliyolengwa na shambulizi la kigaidi, Nairobi, Kenya, Januari 17, 2019. © REUTERS/Njeri Mwangi

Saa 24 baada ya kumalizika kwa shambulio dhidi ya hoteli ya kifahari ya DusitD2 jijini Narobi nchini Kenya, polisi inaendelea na msako katika mji mkuu wa Kenya.

Matangazo ya kibiashara

Kundi la wanangambo wa Kiislamu la Al Shabab lilikiri kuhusika na shambulio hilo lililoua watu zaidi ya 20 ikiwa ni pamoja na raia mmoja kutoka Marekani na mwengine kutoka Uingereza.

Kwa mujibu wa vyanzo vya polisi jijini Nairobi operesheni ya vikosi vya usalama imemalizika Jumatano jioni.

Wakati huo huo polisi imesema kuwa imewakamata watu wawili wanaoshumiwa kushirikiana na washambuliaji waliendesha shambulio katika hoteli hiyo.

Kwa mujibu wa polisi mmoja wa washtumiwa hao amekamatwa huko Ruaka, kaskazini mwa Nairobi, ambapo moja ya magaidi anadaiwa kuwa aliishi kabla ya shambulio hilo. Mwengine amekamatwa huko Eastleigh, eneo la mji mkuu Nairobi kunakoishi raia wenye asili ya Somalia. Shirika la kimataifa la Haki za Binadamu la Human Right Watch pia limeshauri serikali kuepuka matumizi yoyote mabaya wakati wa uchunguzi. shiria hilo lisilo la kiserikali limekumbusha kuwa katika siku za nyuma, "Jitihada za Kenya za kukabiliana na kudorora kwa usalama ziligubikwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu," hasa dhidi ya jamii ya raia kutoka Somalia (Somali).

Usalama kwenye mpaka wa Somalia umeimarishwa ili kuzuia kutoroka kwa baadhi ya wahusika katika shambulio hilo. Hoteli ya DusitD2 bado inazingirwa. Idadi ya washambuliaji bado haijulikani. baadhi ya mashahidi wanasema magaidi walikuwa sita wengine wanasema walikuwa saba. hata hivyo wawili wao watakuwa ni raia wa Kenya. Mmoja ni kutoka Limuru kaskazini mwa mji mkuu Nairobi na mwingine ni kutoka Nyeri, katikati ya nchi.

Katika taarifa yao, kundi la Al Shabab limedai kuwa limeua watu 50 wasiokuwa na imani ya dini, likiongeza kuwa jina la shambulio hilo ni "Jerusalemu haitakuwa eneo la Wayahudi". Shambulizi hilo "ni jibu la maelekezo ya kipumbavu ya Donald Trump na uamuzi wake wa kutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israeli," imesema taarifa hiyo. Raia mmoja kutoka Uingereza na Mmarekani mmoja, walionusurika katika shambulizi la 9/11, ni miongoni mwa watu waliouawa katika shambulio hilo dhidi ya hoteli ya DusitD2.