TANZANIA-UFARANSA

Ufaransa: Mazingira rafiki ndio njia pekee ya kuvutia wawekezaji

Mafundi wa kampuni ya Powercorner wakifunga sola kwenye moja ya vijiji nchini Tanzania
Mafundi wa kampuni ya Powercorner wakifunga sola kwenye moja ya vijiji nchini Tanzania http://powercorner.com/

Nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki zimetolewa wito wa kutengeneza sera rafiki za kiuchumi ili kuvutia wawekezaji wa kimataifa hasa kwenye sekta ya nishati ambayo miaka ya hivi karibuni imeonekana kutoa mchango kubwa katika maendeleo ya nchi.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya nishati, balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frederick Clavier amesema kutokana na kuongezeka kwa ushindani katika soko la kimataifa na kukua kwa teknolojia nchi za ukanda na hasa Tanzania hazina budi kurekebisha sera zake ili ziendane na wakati tulipo.

Balozi Clavier amesema uwekezaji kwenye sekta ya nishati ni muhimu kwa nchi zinazoendelea na hasa ukizingatia kuwa nchi nyingi zinalenga kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na kwamba mazingira rafiki ndio yatavutia wawekezaji wengi zaidi.

“Kama tunataka kutengeneza ajira, kama tunataka kuendeleza uwekezaji mpya! Ni jambo la muhimu sana kuwa na sera yakinifu na zinazoaminika kwa uchumi, na ni jambo zuri kwamba hivi leo hata mimi nimeridhishwa kwa sababu mazungumzo na Serikali ya Tanzania ni ya uwazi, na yanaonesha kwangu mimi kwamba tuna matokeo mazuri katika ushirikiano wetu”.

Balozi Clavier amesema kwa uwekezaji wowote kufanikiwa katika nchi ni lazima mamlaka zitengeneze mazingira mazuri na kuepuka kubadilisha Sera zake mara kwa mara bila kushirikisha makampuni yaliyowekeza.

“Lazima uwekezaji unaofanywa na makampuni ya kigeni uwe ni wa kila upande kunufaika na sio upande mmoja ndio unufaike”.

Kwa upande wao makampuni ya Ufaransa ambayo tayari yameanza kufanya kazi nchini Tanzania yanasema mbali na kuridhishwa na mabadiliko ambayo serikali imeendelea kuyatekeleza ni muhimu kwa watunga sera kuisaidia Serikali kubaini vipaumbele katika sekta ya nishati ya mafuta na gesi ili kuondoa sintofahamu kuhusu mustakabali wa uwekezaji kwenye maeneo hayo.

Elias Kilembe ni naibu mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Ufaransa ya Maurel & Prom ambayo inazalisha gesi mkoani Mtwara.

“Kama Mourel & Prom mpaka sasa hivi hatujajua Serikali inataka nini? Na ile hali ya kutoeleweka inafanya uwekezaji kidogo..uwe unasubiri hali ieleweke, hauwezi kuwekeza kwenye kiza. Lakini kwa kiasi kikubwa, kutokueleweka uwekezaji utakuwaje kunafanya makampuni yasitishe, yangongee maelezo zaidi Serikali inataka nini?”

Kilembe ameonya kuhusu kutokuwepo kwa mipango inayoeleweka kwenye sekta ya nishati ya gesi na mafuta akitolea mfano kampuni yao namna inavopitia changamoto katika uzalishaji wa gesi licha ya kuwa kiwango cha uzalishaji kimeongezeka.

“Awali toka mwaka 2006 mpaka 2015 hakukuwa na mauzo ya kutosha, tulipoanza walikuwa wanauza lita za ujazo laki nane za gesi, sasa hivi tunauza lita za ujazo milioni 2 na hii ni kutokana na uzalishaji kluongezeka”.

Tangu serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na rais John Pombe Magufuli iingie madarakani, imefanya mabadiliko makubwa katika sheria zake zinazohusu rasilimali kuanzia kwenye madini, gesi na mafuta, mabadiliko ambayo hata hivyo baadhi ya makampuni yameonesha wasiwasi kiutendaji.

Licha ya wasiwasi kwa baadhi ya wawekezaji, makampuni mengi ya Ufaransa ambayo yamewekeza na yanatarajia kuendelea kuwekeza nchini Tanzania, yamesema yanaridhishwa na mabadiliko haya na kupongeza namna Serikali imekuwa wazi katika kuwashirikisha katika mazungumzo ili kupata muafaka pale ambapo kunaonekana kuna dosari au kutokueleweka.

Kwa upande wa makampuni ambayo yamewekeza kwenye sekta ya nishati Jadidifu, yanasema licha ya changamoto wanazokutana nazo wakati wakitekeleza miradi, wanasema Serikali ya Tanzania imeendelea kuboresha na kuondoa ukiritimba katika upatikanaji wa baadhi ya vibali.

Mpembe Ngwisa ni mkurugenzi wa kampuni ya powerconer inayofanya kazi na kampuni ya Engie ya nchini Ufaransa katika kusambaza umeme wa nishati ya jua vijijini.

“Kutokana na ukubwa wa nchi yetu, kuna maeneo ni gharama kubwa sana kupeleka umeme wa gridi, kuna maeneo kabisa yanaweza kupata umeme wa jua unaojitegemea kwa kutumia hizi mini-gridi bila gharama kubwa na wananchi hawatasubiri muda mrefu. Uwezo utakapopatikana na maeneo yakifikiwa basi itakuwa rahisi kwa mitambo yetu kuhamishwa maeneo mengine ili ule umeme wa gridi ufike”.

Kwa upande wa kampuni ya mafuta ya Ufaransa TOTAL yenyewe kwa upande wake imesema mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki utazinufaisha pakubwa nchi washirika ambazo ni Tanzania na Uganda baada ya kutiliana saini kuanza utekelezaji wa ujenzi wa bomba hilo.

Mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki kati ya Tanzania na Uganda (EACOP)

EACOP ni mradi wa bomba la mafuta ghafi yatakayo safirishwa na kuuzwa nje, bomba hili lina urefu wa kilometa 1,445 ambalo litasafirisha mafuta ghafi ya Uganda kutoka Kabaale – Hoima nchini Uganda kwenda kwenye peninsula ya Chongoleani karibu na bandari ya Tanga nchini Tanzania.

Mradi huu wa bomba la mafuta ghafi (EACOP) unafanya bomba hili kuwa refu zaidi duniani lenye joto.