SUDANI KUSINI-MAZUNGUMZO-SIASA-USALAMA

Mazungumzo ya kuokoa mkataba wa amani yaendelea Sudani Kusini

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir katika Mkutano wa Igad Machi 25, 2017 Nairobi.
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir katika Mkutano wa Igad Machi 25, 2017 Nairobi. SIMON MAINA / AFP

Wawakilishi wa pande zinazotofautiana nchini Sudan Kusini kwa siku ya pili leo, wanakutana jijini Addis Ababa kujaribu kuokoa mkataba wa amani uliotiwa saini mwaka 2018.

Matangazo ya kibiashara

Mkataba huo ulitaka kuundwa kwa serikali ya pamoja kuazia mwezi huu, lakini matumaini yameonekana kudidimia baada ya kiongozi wa upinzani Riek Machar kusema kuwa, hawezi kurudi jijini Juba kwa sasa kwa sababu za kiusalama.

Machar anataka kuundwa kwa serikali hiyo ambayo ilikuwa ianze kazi tarehe 12 mwezi huu, kuahirishwa kwa miezi kadhaa ili kutatua changamoto ambazo anasema zinamfanya kutokuwa tayari kurejea nyumbani.

Mazungumzo ya Addis Ababa yanawaleta pamoja rais Salva Kiir, kiongozi wa waasi Riek Machar pamoja na makundi mengine yaliyotia saini mkataba wa amani wa mwezi Septemba mwaka jana.

Pande hizo zimekuwa zikivutana kuhusu namna ya kutekeleza baadhi ya vipengele vya mkataba wenyewe, likiwemo suala tata la usalama wa Riek Machar mjini Juba na uundwaji wa jeshi la kitaifa.

Taarifa ya Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Afrika Mashariki na Kati IGAD imesema jumuiya hiyo imelazimika kuitisha kikao hiki cha siku mbili ili kupata suluhu itakayowezesha kuundwa kwa Serikali ya kitaifa.