Watu wawili washikiliwa na polisi Mbeya kwa tuhuma za mauaji ya mtoto
Polisi mkoani Mbeya nchini Tanzania, wanashikilia watu wawili kwa kuhusika na mauaji ya mtoto wa miaka sita Rose Japhet, aliyeuawa kutokana na imani za kishirikina.
Imechapishwa:
Kamanda wa Polisi katika mkoa wa Mbeya Ulrich Matei amesema uchunguzi wao umebaini kuwa mtoto huyo aliuawa tarehe 3 mwezi huu kwa kunyongwa na baadhi ya viungo vyake kunyofolewa.
Miongoni mwa watuhumiwa wa mauaji hayo ya kinyama ametajwa kuwa ni Japhet Nguku, baba mzazi wa mtoto huyo.
Inaelezwa kuwa chanzo cha mauji haya ni tamaa ya fedha, na baba ya msichana huyo alikubali kumuua mtoto wake ili kupata Shilingi Milioni tano za Tanzania.
Vyombo vya Habari nchini Tanzania vinaripoti kuwa baba huyo alikubali mtoto wake kuuawa kwa mfanyibiashara aliyetajwa kwa jina la Andrew Mwambuluma ambaye ni mmiliki wa Shule moja ya sekondari.
Serikali ya Tanzania imekuwa ikikemea visa kama hivi vya ukiukwaji wa haki za binadamu, huku wafanyibiasha na wanasiasa wakituhumiwa kuhusika ili kujipatia umaarufu na fedha kwa imani za kishirikina.