KENYA-MASHOGA-HAKI-KIFO-MAHAKAMA

Mwanaharakati maarufu wa mapenzi ya jinsia moja afariki dunia nchini Kenya

Mwandishi mashuhuri wa vitabu na mwanaharakati wa masuala ya mapenzi ya jinsia moja nchini Kenya Binyavanga Wainaina, amefariki duniani akiwa na umri wa miaka 48, baada ya kuugua muda mfupi kwa mujibu wa maelezo ya watu wake wa karibu.

Mwandishi na mwanaharakati wa jinsia moja nchini Kenya Binyavanga Wainaina siku za uhai wake
Mwandishi na mwanaharakati wa jinsia moja nchini Kenya Binyavanga Wainaina siku za uhai wake Luigi Novi/Wikimedia Commons
Matangazo ya kibiashara

Wainaina, alipata umaarufu mwaka 2002 baada ya kushinda tuzo Caine kutokana na harakati zake barani Afrika.

Kifo chake kimetokea wakati Mahakama Kuu nchini Kenya siku ya Ijumaa, ikitarajiwa kutoa hukumu kuhusu kesi iliyowasilishwa na wanaharakati wanaotetea mapenzi ya jinsia moja, kutaka kuondoa kifungu cha sheria kinachoharamisha vitendo vya mapenzi ya jinsia moja nchini humo.

Mapenzi ya jinsia moja hayakubaliwi nchini Kenya, lakini wanaharakati wa mapenzi hayo wana hofu kuwa huenda uamuzi huo ukaahirishwa tena kama ilivyokuwa mwezi Februari.

Kwa sasa, sheria ya kupinga vitendo vya mapenzi ya jinsia moja nchini humo, inaeleza kuwa iwapo mshukiwa atabainika kuhusika, atafungwa jela hadi miaka 14.

Brian Macharia kutoka muungano wa mashoga na wasagaji nchini Kenya ,anasema wana matumaini kuwa Mahakama itatoa uamuzi wa kuwaunga mkono .

Macharia anasema ana imani hiyo kwa sababu kwa muda mrefu, watu wanaojihusishja na mapenzi ya jinsia moja nchini humo, wamekosa haki kwa kunyanyaswa, kutengwa na kutoeleweka.

Kuelekea uamuzi huu wa kihistoria, mataifa 28 kati ya 49 barani Afrika yana sheria zinapinga vitendo au kutambua ndoa za jinsia moja kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch.

Mataifa kama Somalia, Mauritania, Sudan na Kaskazini mwa Nigeria, sheria za Kiislamu zinatumiwa kutoa hukumu kwa watu wanaobainika kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja, wengi wao wakiuawa.

Miaka ya hivi karibuni, Angola, Msumbiji na Ushelisheli, zimeachanana sheria zinazoharamisha mapenzi ya jinsia moja lakini Uganda na Chad zimebadili sheria na kuwa ngumu zaidi.