UGANDA-RWANDA

Uganda na Rwanda zinazungumza kujaribu kutuliza mzozo wa kimipaka

Rais wa Rwanda Paul Kagame akiwa na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni wakati walipokutana tarehe 25 March 2018.
Rais wa Rwanda Paul Kagame akiwa na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni wakati walipokutana tarehe 25 March 2018. Photo: Michele Sibiloni

Maofisa wa Uganda na wenzao wa Rwanda wanafanya mazungumzo ya kidiplomasia kujaribu kutuliza mzozo wa kimipaka kufuatia tukio la mwishoni mwa juma ambapo wanajeshi wa Rwanda wanadaiwa kuwaua watu wawili kwenye mpaka wa Uganda.

Matangazo ya kibiashara

Katibu mkuu wa wizara ya mambo ya nje ya Uganda, balozi Patrick Mugoya, amesema Serikali zote mbili ziko kwenye mazungumzo ya kidiplomasia kujaribu kuepusha mzozo zaidi.

“Ndio, tunazungumza katika ngazi za kidiplomasia. Ndio maana tuliandika barua ya kupinga kitendo kile na hatufikiri kwamba mzozo unaweza kuwa mkubwa zaidi. Kwa hivyo tunazungumza kusaka suluhu muafaka,” alisema balozi Mugoya ambaye alinukuliwa pia na gazeti la Daily Monitor la Uganda.

Balozi Mugoya amesema licha ya Serikali ya Rwanda kujibu barua yao kwa namna walivyojibu, wao wataendelea kufuata njia sahihi za mazungumzo ili kupata muafaka.

Raia wa Uganda Nyesiga Alex na mwenzake raia wa Rwanda Kyerengye John Batista, waliripotiwa kuoigwa risasi na wanajeshi wa Rwanda kwenye umbali wa kilometa 60 ndani ya mpaka wa Uganda baada ya kukataa kukamatwa.

Maofisa kutoka wizara ya mambo ya nje ya Uganda wamesema kuwa wako tayari kukabidhi mwili wa raia wa Rwanda kwenye mpaka wa Katuna.

Serikali ya Rwanda yenyewe imeendelea kukanusha madai kuwa watu hao wawili waliuawa kwenye ardhi ya Uganda, badala yake inasema waliuawa ndani ya ardhi ya Rwanda.

Kwa miezi kadhaa sasa nchi za Rwanda na Uganda zimekuwa hazina uhusiano mzuri baada ya utawala wa Kigali, kuituhumu Uganda kwa kuwateka na kuwaua raia wake pamoja na kuwahifadhi waasi wanaotaka kuipindua Serikali ya rais Paul Kagame.

Uganda kwa upande wake imekanusha tuhuma zinazotolewa na Rwanda ikiituhumu Rwanda kwa kutuma watu kufanya ujasusi.