BURUND-UHURU-SIASA-USALAMA

Burundi yaadhimisha miaka 57 ya Uhuru

Rais Pierre Nkurunziza, Oktoba 6, 2016.
Rais Pierre Nkurunziza, Oktoba 6, 2016. © RFI-KISWAHILI

Wananchi wa Burundi hii leo wanaadhimisha kumbukizi ya miaka 57 toka taifa hilo lilipojipatia uhuru wake toka kwa wakoloni wa Ubelgiji Julai 1, 1962, wakati huu taifa hilo likiendelea kushuhudia mzozo wa kisiasa na usalama.

Matangazo ya kibiashara

Burundi inapitia mgogoro mkubwa wa kisiasa na usalama tangu mwaka 2015, kufuatia uamuzi wa rais Pierre Nkurunziza kuwania kwa muhula wa tatu katika uchaguzi wa urais mwaka 2015.

Mwaka jana rais Nkurunziza aliwashangaza wengi alipotangaza kwamba hatowania kwenye kiti cha urais katika uchaguzi wa mwaka 2020, wakati Katiba iliyopitishwa mwaka 2018 inamruhusu. Kwa upande wa upinzani ulio uhamishoni, wanasema uchaguzi wa 2020 utakuwa hauna umuhimu wowotena hautakomesha mgogoro uliopo.

Siku hii ya leo inafika wakati wanasiasa wengi wa upinzani wakiwa ukimbizini, nje ya nchi, bila kusahau watu zaidi ya 300,000 ambao walitoroka makaazi yao na kukumbilia, wengi wao katika nchi jirani za DRC, Rwanda, Uganda, Kenya, Zambia na Tanzania.

Ijumaa Juni 29 mwaka huu Tume Huru ya Uchaguzi , CENI, imetangaza kuwa Uchaguzi Mkuu nchini humo utafanyika Mei 20, 2020, lakini haijafahamika ikiwa wanasiasa wa upinzani walio uhamishoni watashiriki uchaguzi huo.

Duru ya kwanza ya Uchaguzi Mkuu itafanyika Mei 20 na duru ya pili itafanyika tarehe 19 Juni, kama mshindi katika uchaguzi wa urais hatakuwa amepatikana kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi.

Tayari baadhi ya wanasiasa wa upinzani kutoka muungano wa vyama vinavyojumuika kwenye muungano Cnared wamebaini kwamba wana wasiwasi kuwa uchaguzi huo huenda ukachochea machafuko nchini Burundi.

Hata hivyo katibu wa kitaifa wa chama tawala cha CNDD-FDD anayehusika na masuala ya Habari Nancy Ninette Mutoni, amekaribisha mchakato wa "amani na wazi": "Vyama vya siasa vinashirikiana na vinajiandalia kwa pamoja Uchaguzi huo Mkuu, " amesema Nancy Ninette Mutoni.

"Tuna imani kwamba mchakato huo utakuwa wa amani, na wenye kuaminika na wa wazi, " ameongeza.