BURUNDI-JAMII-SIASA

Maeneo muhimu ya kihistoria yabadilishwa majina Burundi

Rais Nkurunziza akikagua majeshi wakati wa sherehe ya siku ya uhuru, Julai 1, 2016.
Rais Nkurunziza akikagua majeshi wakati wa sherehe ya siku ya uhuru, Julai 1, 2016. Onesphore Nibigira/AFP

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza amechukuwa hatua ya kubadilisha majina ya maeneo muhimu ya kihistoria ya nchi hiyo, majina yaliyowekwa tangu baada ya Burundi kujipatia uhuru Julai 1, 1962 kutoka mikononi mwa wakoloni Ubelgiji.

Matangazo ya kibiashara

Uwanja mkuu ulioko katika mji mkuu wa Bujumbura, na ambao huchezewa mpira na kuandaliwa sherehe za kitaifa,s asa unaitwa Uwanja wa Mashujaa.

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bujumbura sasa umebadilishwa jina na kuitwa Merchior Ndadaye, rais wa kwanza kutoka jamii ya Wahutu aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, ambaye aliuawa Oktoba 21, 1993.

Ikulu mpya ya rais iliyogharimu dola milioni 22 sawa na (£19m) na ujenzi wake ulikuwa zawadi kutoka China) sasa imepewa jina la mfalme Ntare Rushatsi.

Barabara kuu ya Septemba 3, ambayo ni barabara maarufu nchini Burundi, tarehe inayoashiri siku ambayo kiongozi wa zamani wa kijeshi Pierre Buyoya alivyomng'oa madarakani ndugu yake rais Jean-Baptiste Bagaza mwaka 1987. Kwa sasa barabara hiyo imepewa jina la Luteni Jenerali Adolphe Nshimirimana, aliye kuwa mkuu wa kitengo cha ujasusi ambaye alikuwa akiogopewa kutokana na jinsi alivyokua akiendesha shughuli zake kwa njia ya kikatili. Aliuawa Agosti 2, 2015, mjini Bujumbura.

Katika hotuba ya maadhimisho ya miaka 57 ya uhuru wa Burundi, rais Nkurunziza alisema mpango wa kubadilisha majina ya maeneo muhimu ya kihistoria nchini Burundi “ni njia moja ya kukabiliana na usaliti”

“Lengo la kubadilisha jina la Uwanja wa Kitaifa wa Soka, Ikulu ya rais pamoja na Uwanja wa ndege wa kimataida wa Bujumbura ni kuwakumbusha Warundi historia yao”, alisema Bw Nkurunziza.

"Hatua hii pia inalenga kufuta majina yaliotokana na kuibuka kwa usaliti na tabia mbaya iliyoletwa na ukoloni," aliongeza.

Hata hivyo wakosoaji wake wanaamini kwamba hatua hiyo inataka kuonyesha jamii ya Wahutu walio wengi nchini humo kuwa rais wao anawajali na kutambua mchango wa jamii hiyo katika taifa hilo ndogo Afrika ya Kati linaloendelea kukumbwa na mgogoro wa kisiasa na usalama.