BURUNDI-UN-USALAMA-SIASA

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa: Tuna wasiwasi kuhusu uchaguzi Burundi

Doudou Diène, Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi kuhusu Burundi.
Doudou Diène, Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi kuhusu Burundi. ONU Info/Florence Westergard

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuwa makini kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 nchini Burundi, kwa mujibu wa tovuti ya Radio ya Umoja wa Mataifa.

Matangazo ya kibiashara

Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi kuhusu Burundi Dudou Diène, amesema wananchi wa Burundi wanaendelea kuishi kwa "hofu kutokana na hali inayojiri kwa sasa, ambapo kila mwananchi anahisi kuwa anaweza kuuawa, kufungwa au kufanyiwa mateso kwa wakati wowote"."

"Wananchi wa Burundi wanaendelea kunyanyasika na kuendelea kusubiri kitakacho wakumba, huku baadhi yao wakilazimika kutoroka makaazi yao" amesema mwanasheria huyo, raia wa Senegal.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi kuhusu Burundi, licha ya kutambua kwamba "Burundi haipo katika hali ya vita ambayo inaweza kusababisha matukio ya vurugu kwa kiasi kikubwa," hata hivyo amebaini kwamba "hali inayojiri nchini Burundi inatisha".

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa pia wanaamini kuwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu umeendelea tangu mwezi Mei 2018, ikiwa ni pamoja na mauaji ya, visa vya watu kupotezwa, kukamatwa na kufungwa kiholela, pamoja na mateso, unyanyasaji, unyanyasaji wa kijinsia, watu kunyimwa uhuru wa kujieleza na uhalifu mwengine.

"Visa vya unyanyasaji wa kijinsia pia vimeripotiwa," wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamebainisha. Wengi wa waathirika walikuwa wanawake na wasichana, na kwa kiwango cha chini wanaume, watoto na watu wazima. Unyanyasaji huo mara nyingi ulichukua sura ya ubakaji kwa makundi, hasa wakati makundi ya watu walipokuwa wakifanya mashambulizi usiku katika nyumba za raia hao, wameongeza wachunguzi.

"Waathiriwa, ambao baadhi yao walikuwa wamerejea nchini Burundi, walilengwa kwa sababu ya kushukiwa kuwa katika moja ya vyama vya upinzani, mmoja wa ndugu zao kuwa katika upinzani au katika kundi la waasi au kama watakuwa wamekataa kujiuunga na chama tawala cha CNDD-FDD au vijana wa chama hicho Imbonerakure, "wamesema wajumbe wa Tume ya Uchunguzi kuhusu Burundi.

Serikali ya Burundi haijazungumza chochote kuhusu madai hayo dhidi yake.