CPJ-MAXENCE MELO-TANZANIA

Mkurugenzi Jamii Forums atunukiwa tuzo ya kimataifa ya kutetea uhuru wa habari duniani

Mkurugenzi Mkuu na Mwanzilishi wa Jamii Forums, Maxence Melo
Mkurugenzi Mkuu na Mwanzilishi wa Jamii Forums, Maxence Melo Allafrica.com

Mkurugenzi mtendaji wa tovuti ya Jamii Forums ametajwa kuwa miongoni mwa washindi wa tuzo ya kimataifa ya kutetea uhuru wa vyombo vya habari duniani mwaka 2019.

Matangazo ya kibiashara

Tuzo hiyo hutolewa na kamati ya kimataifa kwaajili ya ulinzi wa waandishi wa habari CPJ, atakabidhiwa tuzo hiyo mwezi Novemba nchini Marekani.

Taarifa za kutangazwa kwa Melo zimetolewa jana kupitia tovuti ya CPJ na inakuja miaka 13 tangu kuasisiwa kwa mtandao huo mashuhuri wa lugha ya kiswahili duniani.

Melo ameshinda tuzo hiyo sanjari na Patricia Campos Mello kutoka Brazil, Neha Dixit wa India na Lucia Pineda Ubau na Miguel Mora wanaotoka Nicaragua.

Katika taarifa yake CPJ imesema Melo atatunukiwa tuzo hiyo kutokana na kupigania uhuru wa kujieleza kupitia majukwaa ya mitandao ya kijamii.

Tovuti ya Jamii Forums yenye mamilioni ya wasomaji na washirika wa mijadala mbalimbali imejizolea umaarufu kwa kuibua hoja na matukio mbalimbali yenye maslahi kwa Tanzania na CPJ inasema Melo amekuwa akikabiliwa na vikwazo kadhaa kutokana na ujasiri wa kutetea uhuru wa kujieleza kupitia mitandao ya kijamii.

CPJ inasema mwanaharakati huyo amepanda kizimbani mara 81 tangu mwaka 2017 kutokana na uthubutu wake wa kutetea uhuru wa kujieleza nchini Tanzania.

Tangu kutangazwa kushinda tuzo hiyo maelfu ya watanzania wamemiminika kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo Twitter, Facebook na instagram kutoa pongezi kwa mwanaharakati huyo.