TANZANIA-JOHN MAGUFULI-CCM

January Makamba ang'olewa uwaziri nchini Tanzania

January Makamba, Mbunge wa Bumbuli aliyefutwa kazi na Rais John Magufuli
January Makamba, Mbunge wa Bumbuli aliyefutwa kazi na Rais John Magufuli Mwananchi

Rais wa Tanzania, John Magufuli amefanya mabadiliko madogo katika baraza la mawaziri huku akimfuta kazi January Makamba, aliyekuwa  akishikilia wizara ya Mazingira na muungano.

Matangazo ya kibiashara

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na kurugenzi ya mawasiliano ya rais na kutiwa saini na mkurugenzi wake Gerson Msigwa inasema nafasi ya Makamba ambaye ni mbunge wa Jimbo la uchaguzi la Bumbuli Kaskazini mashariki mwa Tanzania inachukuliwa na George Simbachawene, mbunge wa Jimbo la uchagizi la Kibabwe mkoani Dodoma.

Hata hivyo taarifa ya ikulu haijatoa sababu zilizopelekea rais Magufuli kumwondoa kazini Januari Makamba.

Mwezi uliopita Makamba aliongoza kampeni iliyofanikiwa ya kuondokana na matumizi ya mifuko ya rambo nchini Tanzania.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Makamba amesema "Nimepokea mabadiliko yaliyofanywa kwa moyo mweupe kabisa, nitasema siku zijazo" ameandika mwanasiasa huyo akiambatanisha na picha aliyopiga na rais mstaafu wa  awamu ya pili Ally Hassan Mwinyi.

Aidha, Simbachawene anarejea kazini tangu alipojiuzulu uwaziri wa nishati na madini mwaka 2017 baada ya jina lake kutajwa kwenye kashfa ya kuingia mikataba ya madini iliyoigharimu Tanzania.

Vilevile rais Magufuli amemteua Hussein Bashe, mbunge wa Nzega Mjini kuwa Naibu Waziri wa kilimo, sekta inayoajiri mamilioni ya Watanzania.

Makamba anaingia katika orodha ya mawaziri waliofurushwa na rais magufuli, wengine ni Nape Nnauye na Mwigulu Nchemba.