KENYA-AL SHABAB-USALAMA

Vikosi vya Kenya vinaendelea na operesheni ya kuwasaka Al-Shabab

Askari wa Kenya (KDF) baada ya shambulio la Al Shabab dhidi ya Chuo Kikuu cha Garissa, Aprili 2015.
Askari wa Kenya (KDF) baada ya shambulio la Al Shabab dhidi ya Chuo Kikuu cha Garissa, Aprili 2015. CARL DE SOUZA / AFP

Vyombo vya usalama nchini Kenya vinafanya operesheni kwenye eneo la Kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ambako inapakana na nchi ya Somalia, operesheni ambayo inalenga kuwasaka wapiganaji wa Al-Shabab wanaojipenyeza kuingia nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Tangu Julai 20 vikosi vya wanajeshi vimekuwa vikifanya doria kwenye maeneo ya rasi ya Kamboni, Kiunga na Ishakani, huku baadhi ya raia kwenye maeneo hayo wakisema ni kama kuna makataa ya kutotembea usiku licha ya kuwa haijatangazwa.

Kwa mujibu wa idara ya ujasusi nchini Kenya, wapiganaji wa Al-Shabab wanadaiwa kuingia nchi Kenya ili kutekeleza mashambulizi.

Kwa mujibu wa wakaazi wa eneo hilo milio ya risasi na milipuko ya mabomu ilisikika siku ya Jumamosi, bila hata hivyo kujua chanzo cha hali hiyo.

Kwa mujibu wa mashahidi , Jeshi la Ulinzi la Kenya, Kenya Defense Forces (KDF) limewataka wakaazi wa maeneo hayo kutokwenda mbali na makaazi yao.

Operesheni hii inakuja kufuatia mfululizo wa mashambulizi yaliyotokea wiki mbili zilizopita.

Mnamo Julai 15, mapigano kati ya wapiganaji wa Al-Shabab na vikosi vya ulinzi vya Kenya yalisababisha wapiganaji watatu wa kundi hilo kuuawa na askari wawili wa Kenya kujeruhiwa.

Uhasama huu hutokea mara kwa mara katika eneo hilo, hasa tangu jeshi la Kenya kutumwa kusaidia nchini Somalia mnamo mwaka 2011.