BURUNDI-HAKI

Mahakama ya Rufaa Burundi yathibitisha kifungo cha miaka 32 dhidi ya Germain Rukuki

Mawakili wakiandamana mbele ya Mahakama Kuu jijini Bujumbura Julai 25, 2011.
Mawakili wakiandamana mbele ya Mahakama Kuu jijini Bujumbura Julai 25, 2011. Photo AFP/Esdras Ndikumana

Mahakama ya rufaa jijini Bujumbura, Burundi imethibitisha adhabu ya kifungo cha miaka 32 jela aliyokuwa amepewa mwanaharakati na mtetezi wa haki za binadamu, Germain Rukuki.

Matangazo ya kibiashara

Rukuki ambae alikamatwa akiwa nyumbani kwake miaka 2 iliyopita, kabla ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 32 mwezi April mwaka 2018 kwa tuhuma za uhaini na kuhatarisha usalama wa taifa, ameendelea kusisitiza kutokuwa na hatia.

Mahakama ya mwanzo ilimhukumu kifungo cha miaka 32 jela baada ya kukutwa na hatia ya kushiriki katika maandamano dhidi ya rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza wakati akiwania muhula wa tatu.

Germain Rukuki anatuhumiwa kushiriki katika vuguvugu lililojaribu mapinduzi ya kijeshi na utekelezwaji wa mauaji ya askari polisi Mei 13 mwaka 2015, tarehe ambayo kundi la wanajeshi waliojaribu bila mafaanikio kumpindua rais Nkurunziza.

Alifungwa tangu Julai 13, 2017, akishutumiwa "kujaribu kuhatarisha usalama wa nchi " na "uasi" kwa kushirikiana na shirika la haki za binadamu la Acat-Burundi, ambalo lilipigwa marufuku nchini Burundi kama mashirika mengi ya haki za binadamu nchini humo.

Awali Mwendesha mashitaka aliongeza makosa mapya katika kesi hiyo - mauaji, uharibifu wa mali ya umma, jaribio la kupindua utawala uliochaguliwa kidemokrasia, makosa ambayo upande wa utetezi haukuweza kufahamishwa. Hali hiyo ilipelekea wanasheria wa mwanaharakati huyo kuomba kesi inayomkabili mteja wao iahirishwe.

Vyombo vya sheria nchini Burundi vinatuhumiwa kwa kutotenda haki dhidi ya watuhumiwa huku kesi ya Germain Rukuki ikiwelezwa kuendeshwa bila ya uwepo wa ushahidi wa kutosha.

Mashirika kadhaa ya kutetea haki za binadamu yanasema hayakushangazwa na uamuzi wa mahakama ya Burundi.

Shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International linabaini kwamba kesi inayomkabiliwa Bw Rukuki na ile inayowakabili wenzake wanne au wanaharakati wa zamani waliofuatiliwa katika kesi zingine inaonyesha utayari wa serikali ya Bujumbura kukandamiza anayethubutu kuikosoa.