RWANDA-UGANDA-USHIRIKIANO

Rwanda yaishtumu Uganda kuwakamata raia wake

Rais wa Rwanda Paul Kagame aendelea kuinyooshea kidole cha lawama Uganda kunyanyasa raia wake.
Rais wa Rwanda Paul Kagame aendelea kuinyooshea kidole cha lawama Uganda kunyanyasa raia wake. REUTERS/Eric Vidal

Rwanda kupitia ubalozi wake nchini Uganda, umeiandikia barua serikali ya Uganda, kulalamikia madai ya kukamatwa kwa raia wake 40 na maafisa wa kijeshi jijini Kampala.

Matangazo ya kibiashara

Vyombo vya usalama vya Uganda vinasema raia hao wa Rwanda, wanashukiwa kuifanyia ujasusi serikali ya Rwanda.

Serikali ya Uganda inadai kwamba Kigali ina njama za kupindua utawala wa Yoweri Museveni kabla ya uchaguzi mkuu wa 2021.

Balozi wa Rwanda nchini Uganda Frank Mugambage amesema kuwa ukamataji huo ni dhihaka.

Magazeti nchini Uganda siku ya Jumatano, yaliandika taarifa kuhusu namna maafisa wa jeshi wakishirikiana na polisi, walivyowakamata raia hao wa Rwanda ndani ya Kanisa moja katika mtaa wa Kibuye jijini Kampala.

Raia hao 40 wa Rwanda, walikamatwa katika Kanisa la Pentecostal Association Churches of Rwanda ADEPR, jijini Kampala.

Rwanda imeendelea kulalamikia kukamatwa na kuteswa kwa raia wake jijini Kampala bila ya makosa yoyote, huku Uganda ikisema operesheni hizo ni za kiusalama, suala ambalo limeendelea kutikisa uhusiano kati ya mataifa hayo jirani.