SUDANI KUSINI-USALAMA-SIASA

IGAD yataka kufanyika kwa mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Salva Kiir na Riek Machar

Rais wa Sudani Kusini Salva Kiir (kulia) akipeana mkono na mpinzani wake Riek Machar, Julai 7, 2018.
Rais wa Sudani Kusini Salva Kiir (kulia) akipeana mkono na mpinzani wake Riek Machar, Julai 7, 2018. SUMY SADURNI / AFP

Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Afrika Mashariki (IGAD) imemuomba rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir kuanza kugawa kiasi cha dola za Marekani milioni 100 kilichoahidiwa kama sehemu ya kuratibu utekelezwaji wa mkataba wa amani.

Matangazo ya kibiashara

Jumuiya ya IGAD ambayo ilifanikisha kupatikana kwa makubaliano ya amani, imeuomba utawala wa Juba kuwa wazi na kuweka mchakato maalumu wa uwajibikaji katika matumizi ya fedha za kuratibu utekelezwaji wa mkataba wa amani.

IGAD pia imewataka rais Salva Kiir na hasimu wake Dr Riek Machar kupanga kuwa na mazungumzo ya ana kwa ana ili kupata suluhu ya masuala tata yaliyosalia ili kuanza utekelezaji wa mkataba wenyewe.

Awali Serikali ilikuwa imeahidi kuanza kutoa fedha inayohitajika kutekeleza mkataba huo, lakini mpaka sasa haijafanya hivyo.

Tume maalumu inayosimamia utekelezwaji wa mkataba wa amani nchini Sudan Kusini imeripoti kuwa kati ya mwezi April na Julai ni dola za Marekani milioni 6.5 tu ndizo zilitolewa kwa ajili ya usalama.