RWANDA-MSUMBIJI-USALAMA

Raia kutoka Rwanda auawa kwa kupigwa risasi Msumbiji

Louis Baziga, ambaye amekuwa mkuu wa jamii ya Wanyarwanda waishio nchini Msumbiji aliuawa Jumatatu asubuhi Agosti 26, 2019 na kundi la watu wasiojulikana waliojihami kwa bunduki.
Louis Baziga, ambaye amekuwa mkuu wa jamii ya Wanyarwanda waishio nchini Msumbiji aliuawa Jumatatu asubuhi Agosti 26, 2019 na kundi la watu wasiojulikana waliojihami kwa bunduki. The New Times (Rwanda)/twitter.com

Mfanyabiashara mkuu wa Rwanda, ambaye pia alikuwa kiongozi wa jamii ya Wanyarwanda nchini Msumbiji ameuawa kwa kupigwa risasi katika mji mkuu Maputo.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa balozi wa Rwanda nchini Msumbiji, Claude Nikobisanzwe, akinukuliwa na idhaa ya maziwa makuu ya BBC (BBC Gahuzamiyrango), waliompiga risasi Baziga, walitoweka kabla ya kutambulika.

“Bwana Baziga alifariki njiani alipokuwa akisafirishwa hospitali. Siwezi kusema ni nani amehusika na kifo hicho, lakini uchuzi umeanzishwa, “ amesema balozi Nikobisanzwe.

“Hii sio mara ya kwanza Baziga kuwahi kulengwa. Aliponea jaribio la kumuua lililotekelezwa na wakaazi wa kutoka Rwanda nchini humo msumbiji mnamo 2016, “ ameongeza balozi wa Rwanda nchini Msumbiji.

Polisi katika mji wa Maputo wanasema Louis Baziga alikuwa ndani ya gari lake Jumatatu mchana baada ya kuondoka nyumbani kwake Matola wakati alipozuiwa na kulpigwa risasi na kundi la watu waliojihami kwa bunduki.

Baziga alifahamika kuwa mfuasi wa serikali ya Rwanda na alikuwa mfanyabiashara maarufu aliyemiliki maduka ya jumla na duka la kuuza dawa mjini Maputo.

Kifo chake kinafuata kile cha Kanali Patrick Karegeya, aliyeuawa katika hoteli moja mjini Johannesburg mnamo 2014.

Na kile cha Camir Nkurunziza, aliyekuwa mlinzi wa kitengo cha ulinzi wa rais, ambaye alipigwa risasi mjini Cape Town mnamo mwezi Mei.