UGANDA-DRC-EBOLA-AFYA

Msichana kutoka DRC apatikana na virusi vya Ebola Uganda

Eneo la mpakani Mpondwe, kati ya DRC na Uganda, Juni 13, 2019.
Eneo la mpakani Mpondwe, kati ya DRC na Uganda, Juni 13, 2019. REUTERS/James Akena

Msichana wa miaka 9 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amepatikana na virusi vya Ebola nchini Uganda, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Uganda.

Matangazo ya kibiashara

Msichana huyo aliwasili nchi Uganda akitokea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya congo. Kwa mujibu wa afisa mmoja wa Uganda ambaye hakutaja jina lake msichana huyo anaendelea kuhudumiwa kwa matibabu baada ya kuthibitika kuwa ameambukizwa virusi vya Ebola.

Msichana huyo aliwasili katika eneo la mpakani la Mpondwe, kwenye mpaka kati ya DRC na Uganda Jumatano wiki hii kutafuta msaada wa matibabu katika mji wa Bwera, Wilayani Kasese, Kusini Magharibi mwa Uganda, Wizara ya Afya ya Uganda imesema katika taarifa. Wizara ya Afya ya Uganda imeongeza kwamba msichana huyo alifanyiwa uchunguzi na vipimo mbalimbali, na kudhihirika kwamba hajawahi kukutana wala kugusana na mtu yeyote kwa upande wa Uganda.

"Msichana huyo alikaguliwa na kufanyiwa vipimo na timu yetu inayosimamia eneo la mpaka wa Mpondwe. Wakati alipokuwa akifanyiwa vipimo, alionekana na dalili za virusi vya Ebola na aliondolewa mara moja sehemu hiyo. Tuna gari la wagionjwa mahututi (ambulensi) ambalo limekabidhiwa timu hiyo. Sampuli za damu zilichukuliwa na kupelekwa Kampala kwa uchunguzi zaidi. Alhamisi wiki hii, matokeo yamethibitisha kwamba msichana huyo aliambukizwa virusi vya Ebola, " amesema Irene Nakasita, afisa wa mawasiliano wa shirika la Msalaba Mwekundu nchini Uganda.

"Hakuna mtu atakayeingia nchini Uganda akiwa na virusi vya Ebola," ameongeza Irene Nakasita.

Mnamo mwezi Juni, watu watatu kutoka familia moja walifariki dunia nchini Uganda baada ya kuambukizwa virusi vya Ebola nchini DRC.

Kulingana na ripoti ya shirika la Afya Duniani (WHO), hadi Agosti 28 nchini DRC, visa 3004 vya maambukizi ya virusi vya Ebola vilithibitishwa na watu 1998 walifariki dunia baada ya kuambukizwa virusi vya Ebola.