Pata taarifa kuu
BURUNDI-UN-USALAMA-SIASA

Ripoti ya Umoja wa Mataifa: "Hali ya hofu" yatawala Burundi miezi michache kabla ya uchaguzi

Mji mkuu wa Burundi, Bujumbura.
Mji mkuu wa Burundi, Bujumbura. © AFP/Carl de Souza

Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi imebaini katika ripoti yake kwamba "hali ya hofu" inatawala katika nchi hiyo, ikiwa imesalia miezi minane kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Matangazo ya kibiashara

Katika ripoti yake, Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi, iliyoundwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 2016, inaelezea jinsi mamlaka nchini humo na vijana wa chama tawala, Imbonerakure, wanaendelea kuwafanyia vitisho raia kwa kuwalazimisha kujiunga, kuunga mkono au kuchangia chama tawala, CNDD-FDD.

"Leo nchini Burundi, ni hatari sana kukosoa utawala," amesema mwenyekiti wa kamati hiyo, Doudou Diene, akinukuliwa katika taarifa.

Ripoti hiyo inaelezea "hali hii ya uoga na vitisho" na jinsi vijana wa chama tawala, Imbonerakure, walivyojihusisha na mauaji, visa vya watu kutoweka, visa vya watu kukamatwa kiholela na visa vya watu kuzuiliwa bila hatia yoyote, visa vya watu kuteswa na ubakaji dhidi ya wafuasi wa vyama vya siasa vya upinzani, au dhidi ya watu wanaoshukiwa kuwa katika vyama vya upinzani.

Duru ya kwanza ya uchaguzi wa urais, ambao umepangwa kufanyika Mei 20 mwaka ujao, imejumuisha uchaguzi wa wabunge na ule wa serikali za mitaa, wakati duru ya pili ya uchaguzi wa urais umepangwa kufanyika Juni 19 na rais mpya ataapishwa Agosti 20.

Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa inabaini kwamba kiwango cha kutisha cha vurugu nchini Burundi kinachochewa na tabia ya kutowaadhibu wahalifu.

Burundi inaendelea kukumbwa na mgogoro wa kisiasa tangu Rais Pierre Nkurunziza atangaze nia yake ya kuwania katika uchaguzi wa urais mwezi Aprili 2015 kwa muhula wa tatu. Alichaguliwa tena mnamo mwezi Julai mwaka huo huo.

Vurugu na ukandamizaji pamoja na mzozo huo vimesababisha vifo vya watu wasiopungua 1,200 na zaidi ya watu 400,000 walitoroka makazi yao kati ya mwezi Aprili 2015 na mwezi Mei 2017, kwa mujibu wa Mahakama ya Jinai ya Kimataifa, ambayo imeanzisha uchunguzi kuhusu hali inayoendelea Burundi.

Wakati huo huo shirika la haki za binadamu nchini Burundi Ligue Iteka limebaini kwamba watu 264 wameuawa tangu mwanzoni mwa mwaka huu nchini humo.

Serikali ya Burundi haijazungumza chochote kuhusu tuhuma hizi.

Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.