KENYA-MAREKANI-UN-ELIMU

Mwalimu bora duniani Mkenya Peter Tabichi akutana na rais Trump

Rais wa Marekani Donald Trump alipokutana na Mwalimu bora duniani, Mkenya Peter Tabichi
Rais wa Marekani Donald Trump alipokutana na Mwalimu bora duniani, Mkenya Peter Tabichi COURTESY: TWITTER/Stephanie Grisham

Rais wa Marekani Donald Trump amekutana na Mwalimu Peter Tabichi, raia wa Kenya aliyeshinda tuzo ya kila mwaka ya Mwalimu bora duniani.

Matangazo ya kibiashara

Tabichi alikutana na rais Trump katika Ikulu ya Marekani jijini Washington DC.

Trump amempongeza Mwalimu Tabichi kwa jitihada na mchango wake wa kuwasaidia wanafunzi kutoka familia masikini nchini Kenya.

Tabichi, ni mtawa wa shirika la kikatoliki la Mtakatifu Fransisco wa kapuchini ni Mwalimu wa Sayansi katika Shule ya Sekondari ya Keriko katika Kaunti ya Nakuru.

Alishinda tuzo hiyo kutokana na jitihada zake za kutumia asilimia 80 ya mshahara wake kuwalipia wanafunzi kutoka familia masikini.

Mwalimu huyo bora duniani amesema kukutana na rais Trump, imekuwa kama ndoto kwake.

“Ilikuwa kama ndoto. Nilipokea mwaliko kutoka Ikulu ya White House, na baada ya kupekuliwa na maafisa wa usalama, niliruhusiwa kuonana na rais Trump,” alisema Tabichi.

Aidha, amesema katika kikao hicho cha dakika 15, Trump alimuuliza maendeleo ya elimu barani Afrika na nchini Kenya.

Mbali na ziara hiyo katika Ikulu ya White House, atahuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu elimu jijini New York.