SUDAN-SUDAN KUSINI-KIIR-MACHAR

Rais Kiir aonya kuunda serikali ya pamoja bila ya mpinzani wake Riek Machar

Rais wa Sudan Kusini  Salva Kiir
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir REUTERS/Andreea Campeanu

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir, ameonya kuwa huenda akalazimika kuunda serikali ya pamoja iwapo kiongozi wa upinzani Riek Machar hatarejea jijini Juba hivi karibuni.

Matangazo ya kibiashara

Kiir ameyasema hayo jijini Juba, wakati wa maombi ya kitaifa kuadhimisha mwaka mmoja baada ya kutiwa saini kwa mkataba wa amani .

“Nawaahidi kuwa, ifikapo Novemba, serikali ya pamoja ni lazima iundwe.Iwapo wapinzani hawataki, kuunda serikali nasi, sisi tutaendelea na kuunda serikali hii kwa wakati,” amesema rais Kiir.

“Hata akija mwezi Oktoba, sina shida, acha aje,” aliongeza Kiir.

Mkataba huo ulimaliza mapigano ya miaka mitano, yaliyosababisha vifo vya maelfu ya watu na mamilioni kuyakimbia makwao.

Rais Kiir na Machar baada ya kutia saini mkataba huo, walilkubaliana kuunda serikali ya mpito haraka iwezekanavyo lakini hilo halijafanikiwa.

Hata hivyo, wiki mbili zilizopita, rais Kiir na Machar walikutana jijini Juba na kuonana ana kwa ana na kukubaliana kuwa serikali hiyo ya pamoja, itaundwa mwezi Novemba.

Kiir amemtaka Machar ambaye ambaye anaishi katika nchi jirani ya Sudan, kurejea Juba mapema.