TANZANIA-HRW-AI-HAKI-USALAMA

Utawala wa Magufuli wanyoshewa kidole

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli Dar es Salaam, Oktoba 30, 2015.
Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli Dar es Salaam, Oktoba 30, 2015. REUTERS/Sadi Said

Watetetezi wa haki za binadamu wanaishtumu serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuminya uhuru wa vyombo vya Habari, na masharika ya kiraia, suala ambalo wanasema linarudisha nyuma uhuru wa kidemokrasia nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Mashirika mawili ya Kimataifa ya kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch na Amnesty International, yametoa ripoti zao leo jijini Nairobi nchini Kenya, yakisema haki za binadamu nchini Tanzania zinakiukwa chini ya utawala wa rais John Magufuli. Ripoti hizo zimetaja kutoweka na kukamatwa kwa wanaharakati na wapinzani wa serikali, akiwemo mwanahabari Azory Gwanda, ambaye alitoweka mwaka 2017 na hadi sasa hajulikani alipo, pamoja na Erick Kabendera ambaye anazuiwa gerezani pamoja na magazeti kadhaa kufungwa.

Mtafiti wa Amnesty International, Roland Ebole, amesema kwa kipindi kirefu, kinachoendelea nchini humo hakikuwahi kushuhudiwa, katika nchi wanayosema miaka iliyopita, kulikuwa na uhuru wa kuongea na wanahabari kuripoti matukio mbalimbali.

Human Rights Watch na Amnesty International, zinasema zimelazimika kutoa ripoti zao kutoka jijini Nairobi, baada ya kukosa idhini ya kufanya hivyo.

Ripoti hii imekuja, wakati huu Tanzania ikielekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi Novemba, na baadaye Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, uchaguzi ambao rais Magufuli anatarajiwa kuwania tena.

Hata hivyo, ripoti kama hizi zimekuwa zikikanushwa vikali na serikali nchini humo.