KENYA-JAJI-MAHAKAMA-BAJETI

Jaji Mkuu wa Kenya aishtumu serikali kwa kukwamisha shughuli za Mahakama

Jaji Mkuu wa Kenya David Maraga, Novemba 04 2019
Jaji Mkuu wa Kenya David Maraga, Novemba 04 2019 Kenya Judiciary

Jaji Mkuu wa Kenya David Maraga, amemshutumu rais Uhuru Kenyatta kwa kujaribu kudhibiti shughuli za Mahakama nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Maraga ametoa kauli hii, baada ya serikali kuamua kuipunguzia bajeti ya fedha, suala ambalo amesema linatishia utendakazi wa muhimili huo muhimu, huku akihoji ni kwanini Mahakama inaingiliwa.

“Kila mtu asimamie jukumu lake, kwanini wanatupunguzia fedha ? Lengo ni kujaribu kuingilia majukumu yetu,” alisema Jaji Maraga.

Akionekana mwenye hasira wakati akizungumza na Wanahabari jijini Nairobi, Maraga amesema hatua ya Mahakama kutokuwa na fedha za kutosha, zimesababisha Majaji wa Mahakama ya rufaa, kushindwa kufanya kazi zao katika miji minne na hivyo kulazimika kusitisha vikao vyao.

“Iwapo bajeti haitaangaliwa upya, hatuna fedha za kununua mafuta kwa ajili ya nagari yanayowasafirisha Majaji, na inamaanisha kuwa hatutakuwa na kesi zitakazosikilizwa na Majaji wa Mahakama ya rufaa,” alisema.

“Mahakama maalum zinazoshughulikia kesi za ufisadi, zitasitisha shughuli zake,” aliongeza.

Jaji huyo ambaye pia ni rais wa Mahakama ya Juu nchini humo, ameapa kususia shughuli za kiserikali iwapo bajeti katika idara hiyo haitaangaliwa upya.

Wachambuzi wa siasa wanaona kuwa, idara ya Mahakama inapitia masaibu hayo baada ya rais Uhuru Kenyatta kuionya Mahakama mwaka 2017, wakati Mahakama ya Juu ilipofutilia mbali ushindi wake, baada ya Uchaguzi Mkuu.