SUDAN KUSINI-KIIR-MACHAR

Serikali ya Sudan Kusini yataka kura ya maoni itumiwe kuamua mustakabali wa majimbo

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir REUTERS/Jok Solomun

Serikali ya Sudan Kusini mwishoni mwa juma lililopita imesema suala la mgawanyo wa majimbo ambalo linapingwa vikali na upinzani linapaswa kuamuliwa kupitia kura ya maoni.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa baraza la mawaziri Martin Elia Lomuro, amesema rais Salva Kiir aliwaeleza wasiwasi wake kuhusu uwepo wa majimbo 32 na kwamba wasiwasi wake uliungwa mkono na mawaziri wengine wanaotaka kusalia kwa majimbo 32.

Suala la kuongezwa kwa majimbo limekuwa ni sehemu ya mvutano unaokwamisha utekelezaji wa mkataba wa amani uliotiwa saini na pande mbili zinazohasimiana mwaka 2018 na pia kuchelewa kuundwa kwa serikali ya umoja.

Rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar mwezi Novemba, walikubaliana kuunda serikali ndani ya siku 100, baada ya kukutana jijini Kampala nchini Uganda.

Wachambuzi wa masuala ya Sudan Kusini, wanaona kuwa kutokana na historia ya kutoaminiana kwa wawili hawa, huenda serikali hiyo isiundwe kama ambavyo imekuwa ikishuhudiwa tangu mwaka 2018.

Marekani imekasirishwa na hatua ya rais Kiir na Machar kuchelewa kuunda serikali hiyo na kuamua kumrudisha nyumbani balozi wake jijini Juba.