SUDANI KUSINI-KIIR-MACHAR-SIASA-USALAMA

Kiir na Machar wakubali kuunda serikali ya umoja mwishoni mwa mwezi Februari 2020

Kiongozi wa waasi Riek Machar amewasili nchini Sudani Kusini ambapo alikutana na Rais Salva Kiir kwa mara ya pili tangu mwezi Septemba kwa lengo la kuandaa kurudi kwake nchini Sudani Kusini.
Kiongozi wa waasi Riek Machar amewasili nchini Sudani Kusini ambapo alikutana na Rais Salva Kiir kwa mara ya pili tangu mwezi Septemba kwa lengo la kuandaa kurudi kwake nchini Sudani Kusini. ALEX MCBRIDE / AFP

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar wamejikubalisha kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kabla ya mwisho wa mwezi wa Februari mwakani, baada ya kumalizika kwa siku 100 waliyopewa na viongozi wa ukanda huo.

Matangazo ya kibiashara

"Tumejikubalisha wenyewe kwamba ltunapaswa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa baada ya siku 100," amesema Salva Kiir baada ya mkutano na Riek Machar, ambaye kwa upande wake amesisitiza kwamba swali la idadi ya majimbo, ambalo limekuwa likizua mtafaruku mkubwa katika mazungumzo, bado halijapatiwa ufumbuzi.

Riek Machar, ambaye anaeshi uhamishaji jijini Khartoum, nchini Sudan, amesema pande zinazojadili zinasubiri ripoti kutoka kwa Makamu wa Rais wa Afrika Kusini David Mabuza kabla ya kuendelea na suala hilo.

Salva Kiir amesema kuwa ikiwa suala la idadi ya majimbo litakuwa halijapatiwa ufumbuzi hadi wakati wa uundwaji wa serikali, serikali hiyo mpya ndio itahusika na kutafutia ufumbuzi swala hilo, pamoja na maswala mengine ambayo yatakuwa bado hayajapatiwa ufumbuzi. Hata hivyo wawili hao wameafikiana kuhusu kuingizwa kwa jeshi na polisi kwa wapiganaji kutoka kambi zote mbili, suala jingine muhimu katika mazungumzo yanayoendelea. "Tunataka kuanza kutoa mafunzo kwa vikosi mbali mbali vya usalama ndani ya kipindi cha wiki moja au mbili," amesema Riek Machar.

Tangu kusainiwa kwa makubaliano ya amani mnamo mwezi Septemba 2018, mapigano yamepungua sana nchini Sudani Kusini, lakini Salva Kiir na makamu wake wa zamani, Riek Machar, wameshindwa kutekeleza vifungu kadhaa muhimu vya makubaliano, pamoja na uundaji wa jeshi moja, lakini pia mpangilio wa mipaka na idadi ya majimbo nchi humo.

Katika muktadha huu, zoezi la kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, lililokuwa lilipangwa hapo awali mwezi Mei, liliahirishwa kwa mara ya kwanza hadi Novemba 12. Kisha tarehe mpya ya siku 100 ilitolewa kwa mahasimu hao wawili, wakati wa mkutano nchini Uganda ambapo washirika wa kikanda (Kenya, Uganda na Sudan haswa) walishiriki.

Sudani Kusini ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo 2013, miaka miwili baada ya kupata uhuru wake kutoka Sudani, wakati Salva Kiir, kutoka jamii ya Dinka, alimshtumu Riek Machar, makamu wake wa zamani wa rais, kutoka jamii ya Nuer, kwa kupanga mapinduzi. Mzozo huo umewaua zaidi ya watu 380,000.