KENYA-MAREKANI-Al SHABAB-USALAMA

Kenya: Jeshi la Marekani laimarisha ulinzi baada ya shambulio dhidi ya kambi yao

Wanajeshi wa Marekani watumwa Kenya (picha ya kumbukumbu)
Wanajeshi wa Marekani watumwa Kenya (picha ya kumbukumbu) © SIMON MAINA / AFP

Shambulio la Jumapili asubuhi katika kambi ya jeshi Mashariki mwa Kenya liliuwa Wamarekani watatu na kupelekea Washington kuimarisha ulinzi katika eneo hilo.

Matangazo ya kibiashara

Marekani imebaini kwamba tayari imetuma kikosi cha askari wake cha EARF, East Africa Response Force, tangu Jumapili.

Kwa mujibu wa Meja Jenerali William Gayler wa kutoka makao makuu ya jeshi la Marekani barani Afrika, wanajeshi hawa, ambao idadi yao haijulikani, "ni kikosi cha kupambana chenye uwezo wa kutumwa haraka. Ni kikosi chenye nguvu yenye uwezo usioepukika inapohitajika, "afisa huyo amesema.

Kikosi hiki kinahusika katika operesheni mbali mbali za kijeshi, ikiwa ni pamoja na ulinzi wa raia wa Marekani na majengo ya serikali ya marekani.

Kikosi hiki kiko chini ya usimamizi wa jeshi la Marekani katika Pembe la Afrika, lenye makao yake makuu Djibouti.

Akiwa jijini Nairobi, mshauri wa usalama Andrew Franklin ameeleza kwamba "askari hawa wapo ili kulinda eneo hilo iwapo kutakuwa na shambulio jipya.

"Jukumu lao ni kutathmini na kulinda. Sio kikosi ambacho kitapigana moja kwa moja na wapiganaji wa KIiislamu wa Al Shabab, " ameongeza Franklin.