SUDANI KUSINI-SIASA-USALAMA

Serikali ya Umoja kuundwa Februari 22 Sudan Kusini

Salva Kiir baada ya mkutano na Riek Machar ambapo wawili hao  walifikia makubaliano ya kuunda serikali ya umoja, huko Juba, Desemba 17, 2019.
Salva Kiir baada ya mkutano na Riek Machar ambapo wawili hao walifikia makubaliano ya kuunda serikali ya umoja, huko Juba, Desemba 17, 2019. REUTERS/Jok Solomun

Serikali ya Umoja inatarajiwa kuundwa nchini Sudan Kusini tarehe 22 mwezi ujao, lakini suala tata la kutatua mzozo wa idadi ya majimbo na mipaka yake, huenda likasuburi serikali hiyo kwa mujibu wa wasuluhishi wa mzozo huo ambao ni IGAD na Umoja wa Afrika.

Matangazo ya kibiashara

Kinara wa tume hiyo maalum ya umoja wa Afrika na  Jumuiya ya Maendeleleo ya Kiuchumi Mashariki mwa Afrika IGAD , Makamu wa rais wa Afrika Kusini, David Mabuza, amesema maswala mengi yanatarajiwa kutafutiwa ufumbuzi na serikali ijayo.

“Sote tumekubaliana kuwa kutaanzishwa serikali ya umoja wa kitaifa lakini swala la idadi ya majimbo yatakayokuwepo nchini litatatuliwa siku tisini baada ya kuanzishwa kwa serikali hiyo” ,amesema David Mabuza.

 “Habari nzuri ni kwamba lile pendekezo la kuanzisha serikali ya umoja wa kitaifa kwanza kabla ya kutatua swala la idadi ya majimbo, halijapingwa na serikali ya rais Salva Kiir” , ameongeza Bw Mabuza., huku akibaini kwamba wanatarajia kukamilisha pendekezo hilo na watafahamisha “wananchi wa Sudan Kusini mara tu litakapokamilika.”

Hayo yanajiri wakati Marekani imeendelea kuweka shinikizo kwa rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na kiongozi wa kivita, makamu wake wa zamani Riek Machar, kutafutia suluhu matatizo yanayosalia.