UGANDA-SIASA-POLISI-BESIGYE

Uganda: Mwanasiasa wa upinzani Kizza Besigye azuiwa na polisi

Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye
Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye RFI/Charlotte Cosset

Polisi nchini Uganda imemuachia huru mwanasiasa wa upinzani nchini humo Kizza Besigye baada ya kumzuia kwa saa kadhaa katika kituo cha polisi cha Nalufenyaa baada ya kukamatwa mjini Jinja ambako alikuwa awe na mkutano wa kisiasa.

Matangazo ya kibiashara

Kabla ya kukamatwa, kwa saa kadhaa Besigye na wafuasi wake walikabiliana na polisi kabla ya kutumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kukabiliana na wafuasi wake.

Kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter, Besigye amechapisha picha zinazoonesha namna polisi walivyotumia nguvu kuwakabili wafuasi wake wakati akijiandaa kwa mkutano wa maadhimisho ya miaka 15 tangu kuundwa kwa chama cha FDC.

Polisi nchini Uganda wamekuwa wakituhumiwa kutumia nguvu kupita kiasi wanapokabiliana na wafuasi wa Besigye au wale wa mwanasiasa kijana na mwanamuziki Bob Wine.

Uganda inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2021, na rais Yoweri Museveni anatarajiwa kutetea wadhifa huo, licha ya kuwa madarkani kwa zaidi ya miaka 30.