TANZANIA-SIASA-UCHAGUZI-MAGEUZI

Tanzania yakataa shinikizo za kuifanyia mageuzi Tume ya Uchaguzi

Serikali ya Tanzania imekataa shinikizo za wanasiasa wa upinzani wanaotaka mageuzi  ya Tume ya Uchaguzi, kuelekea Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Rais wa Tanzania John Magufuli
Rais wa Tanzania John Magufuli Ikulu/Tanzania
Matangazo ya kibiashara

Chama kikuu cha upinzani CHADEMA kinadai kuwa, Tume ya Uchaguzi ilivyoundwa sasa, sio huru na inaegemea maslahi ya chama tawala CCM, kinachongozwa na rais John Magufuli.

Shinikizo kama hizo pia zimetolewa hivi karibuni na Ubalozi wa Marekani nchini humo, ambao umetoa wito kwa Uchaguzi utakaokuwa huru na haki.

Waziri Mkuu wa nchi hiyo Kassim Majaliwa, amepuuzilia mbali shinikizo hizo za upinzani kwa kile alichosema, Tume hiyo imeundwa kwa mujibu wa katiba ya Tanzania ambayo inaelezea uhuru wake.

“Tume ya Uchaguzi ni huru, na haingiliwi katika majukumu yake, sio hata kutoka kwa rais au chama chochote cha siasa,” alisisitiza Majaliwa.

Siku ya Jumatatu, kiongozi mkuu wa upinzani Freeman Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha Chadema, alisema tume hiyo sio huru kwa sababu rais ana mamlaka ya kuwateua na  kuwafuta kazi Makamishena wanaosimamia shughuli za tume hiyo.

Mwaka 2019, upinzani nchini humo ulijiondoa kwenye Uchaguzi wa serikali za mitaa, baada ya kusema kuwa, zoezi hilo lisingekuwa huru na haki.

Katiba ya Tanzania inaeleza kuwa, Tume ya Uchaguzi ikimtangaza mshindi wa kiti cha urais, ushindi huo hauwezi kupingwa Mahakamani.

Rais Magufuli ambaye alichaguliwa mwaka 2015, anatarajiwa tena kuwania nafasi hiyo kwa muhula wa pili.