RWANDA-UGANDA-USHIRIKIANO

Uganda na Rwanda zaendelea kuimarisha uhusiano wao

Marais wa Rwanda na Uganda, Paul Kagame na Yoweri Museveni, mwaka 2018 huko Entebbbe, Uganda.
Marais wa Rwanda na Uganda, Paul Kagame na Yoweri Museveni, mwaka 2018 huko Entebbbe, Uganda. Michele Sibiloni / AFP

Marais wa Uganda na Rwanda wanatarajia kukutana Ijumaa Februari 21 katika mpaka wa Uganda na Rwanda wa Katuna katika juhudi za kuendeleza mchakato wa kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili, ambao ulikuwa unalega lega.

Matangazo ya kibiashara

Raia wa pande zote mbili wanatarajia marais hao watafungua mpaka wa Gatuna uliofungwa mwezi wa Februari mwaka jana na kurudisisha uhusiano mwema wa mataifa hayo.

Rais Paul Kagame wa Rwanda na mwenzake Yoweri Museveni wa Uganda wamekuwa wakikutana na kuafikiana kuhusu kuimarisha uhusiano kati yao ili kumaliza uhasama uliopo.

Wiki hii Serikali ya Uganda iliwaachia huru raia wengine 13 wa Rwanda waliokuwa wamezuiliwa katika jela zake wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali.

Kwa mjibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Sam Kutesa, raia hao wa Rwanda ni wale waliokamatwa mwaka 2019 kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya kukutwa na silaha.

Hili ni kundi la pili baada ya Wanyarwanda wengine kukabidhiwa mapema mwezi wa Januari mwaka 2020, katika hatua ya kumaliza uhasama uliopo kati ya mataifa hayo.

Rwanda imekuwa ikishtumu Uganda kuwapa hifadhi waasi wanaotaka kuhatarisha usalama wake, akuwafunga kiholela raia wake, huku Uganda ikiishtumu Rwanda kuandaa kundi la watu ili kuhatarisha usalama wake.