SUDAN KUSINI-MACHAR-KIIR

Sudan Kusini: Rais Kiir na Machar waunda serikali ya muungano

Kiongozi wa waasi nchini Sudan Kusini Riek Machar ameapishwa kama makamu wa kwanza wa rais, ikiwa ni uundwaji wa serikali ya muungano na rais Salva Kiir iliyokuwa inasubiriwa kwa muda mrefu, kumaliza vita nchini humo.

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir (Kushoto) na kiongozi wa waasi Riek Machar wakiwa jijini Juba Februari 20 2020
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir (Kushoto) na kiongozi wa waasi Riek Machar wakiwa jijini Juba Februari 20 2020 REUTERS/Jok Solomun
Matangazo ya kibiashara

Hatua hii imepongoezwa na Jumuiya ya Kimataifa na mataifa jirani ya Afrika Mashariki, kama ishara ya kuleta amani nchini humo, huku Marekani ikisema imekaribisha hatua hiyo.

Hafla ya uundwaji wa serikali hii imefanyika jijini Juba na rais Kiir na Machar wemesalimiana huku wakishangiliwa na wageni mashuhuri waliohudhuria kuapishwa kwa Machar na viongozi wengine kutoka vyama vya upinzani.

Rais Kiir amewaambia wananchi wa Sudan Kusini kuwa, vita vimefika mwisho na sasa ni wakati wa amani.

Hii ni mara ya tatu tangu nchi hiyo kuundwa mwaka 2011, rais Kiir na Machar wanaungana kuongoza taifa hilo, na awamu hii imefuatia mkataba wa amani wa mwaka 2018.

Kwa mujibu wa mkataba huo wa amani, rais atakuwa ni mmoja, lakini atakuwa na Makamu watano huku Mawaziri wakiwa 35. Kutakuwa na wabunge 550 huku Magavana wakiwa 10.

Uamuzi wa rais Kiir kukubali kupunguzwa kwa idadi ya majimbo kutoka 32 hadi 10 na Machar kuhakikishiwa usalama, ni miongoni mwa sababu kubwa ambazo zimesaidia ufanikishwaji wa uundwaji wa serikali hiyo.