TANZANIA-VYOMBO VYA HABARI-HAKI

Mwandishi wa habari maarufu Kabendera aachiliwa huru Tanzania

Mwandishi wa habari za uchunguzi nchini Tanzania Erick Kabendera akiwasili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam, Tanzania Agosti 19, 2019.
Mwandishi wa habari za uchunguzi nchini Tanzania Erick Kabendera akiwasili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam, Tanzania Agosti 19, 2019. REUTERS/Emmanuel Herman

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya jijini Dar es salaam imemwachilia huru mwanahabari mpekuzi wa Tanzania, Erick Kabendera na kumwamuru alipefaini na fidia ya jumla ya Shilingi milioni 273 baada ya kukiri makosa yaliyokuwa yanamkabili yakiwemo ya utakatishaji fedha na ukwepaji kodi.

Matangazo ya kibiashara

Mahakama imetoa uamuzi huo leo chini ya usimamizi wa Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega baada ya mwenendo wa kesi iliyokuwa ikimkabili kukamilika kupitia mazungumzo na makubaliano baina yake na Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP).

Hata hivyo Bw Kabendera ameondolewa shitaka la kuongoza genge la uhalifu.

Kabendera amekiri shitaka la kukwepa kulipa kodi ya Shilingi milioni 173, kama ambavyo ameahidi pia kulipa kiasi hicho kwa mafungu ndani ya kipindi cha miezi 6 kuanzia sasa.

Aidha mwandishi huyo maarufu wa habari za uchunguzi amekiri shitaka la utakatishaji fedha na mahakama imeelezwa kwamba, Kabendera tayari amelipa kiasi cha Shilingi milioni 100 kama faini ya shtaka hilo.

Kabendera alipata umashuhuri kwa kuandika makala katika magazeti ya ndani, ya kanda na ya kimataifa yakiwemo ya The Guardian na The Times of London ya nchini Uingereza.

Kabendera alichapisha makala katika magazeti mbalimbali, hususan lile la kanda la The East African akizungumzia kile kinachoelezwa kuwa ni uwepo wa mgawanyiko na mpasuko ndani ya chama tawala CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Kabendera alikamatwa mwezi Julai 2019 , kwa tuhuma za kukwepa kulipa kodi, kutakatisha fedha na kuongoza genge la uhalifu.