Uchaguzi wa urais nchini Burundi: Wagombea sita wakubaliwa kuwania kiti cha urais
Kati ya faili kumi za wagombea zilizowasilishwa kwa uchaguzi wa urais Mei 20 nchini Burundi, sita zimekubaliwa na Tume Huru ya Uchaguzi, CENI. Wagombea ambao faili zao zimekataliwa wana siku mbili za kukata rufaa, amesema Mwenyekiti wa CENI, Dkt Pierre Claver Kazihise.
Imechapishwa:
Hatua hii imewashangaza wengi baada ya kusikia kuwa faili ya aliyekua rais wa Burundi Domitien Ndayizeye katika kipindi cha mpito kati ya mwaka wa 2003 na 2005.
Domitien Ndayizeye leo ni kiongozi wa muungano wa Kira Burundi unaoundwa na vyama vidogo vidogo vya upinzani. Sababu za kukataliwa kwa faili yake bado hazijajulikana.
Wagombea wengine ambao faili zao hazikukubaliwa, ni viongozi wa vyama vidogo vidogo vitatu vya siasa: Anicet Niyonkuru wa chama cha CDP, Jaques Bigirimana wa chama cha FNL na Valentin Kavakure wa chama cha FPN. Wagombea hawa wote sasa wana siku mbili za kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Tume ya Uchaguzi kwa Mahakama ya Katiba.
Faili ya kiongozi wa upinzani, Agathon Rwasa, imekubaliwa. Kwa hivyo ataweza kuwania katika uchaguzi wa urais wa Mei 20, lakini kiongozi huyo wa zamani wa kihistoria wa FNL atapeperusha bendera ya chama cha CNL. Chama chake kilisajiliwa mwaka mmoja uliopita, lakini leo inachukuliwa kama chama cha pili chenye wafuasi wengi nchini.
Bw. Rwasa atakuwa mshindani mkuu wa Jenerali Évariste Ndayishimiye, atakayepeperusha pendera ya chama tawala cha CNDD-FDD katika uchaguzi huo.