EAC-DRC-CORONA-AFYA

Coronavirus: Changamoto za madereva wa malori Afrika Mashariki

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, hivi karibuni alibaini kwamba madereva hao ni chanzo cha wasiwasi kwa Uganda na ukanda mzima.
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, hivi karibuni alibaini kwamba madereva hao ni chanzo cha wasiwasi kwa Uganda na ukanda mzima. REUTERS/James Akena

Kila siku, mamia ya malori huondoka bandari kuu za Afrika Mashariki, hususan nchini Kenya na Tanzania zikisheheni bidhaa katika mataifa ya jumuiya ya Afrika Mashariki, na kuzusha hofu kwamba madereva wa malori ndio wasambazaji wakuu wa virusi vya Corona.

Matangazo ya kibiashara

Wakati nchi nyingi za ukanda huo zimeweka marufuku ya raia kutotembea ili kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona, madereva wa malori ni miongoni mwa wachache wanaoweza kusafiri na kupeleka bidhaa, hususan chakula, katika nchi mbalimbali za jumuiya hiyo.

Hivi karibuni malori zaidi ya 300 yalikwama katika mpaka wa Namanga unaoziunganisha nchi za Kenya na Tanzania. Kundi la madereva wa magari makubwa ya kubeba mizigo linatajwa kusambaza virusi vya Corona kwa kiwango cha juu.

Lakini vipimo vilivyofanywa kwenye vituo vya mipakani vimeonyesha idadi kubwa ya visa vya maambukizi miongoni mwa madereva hao na kuonyesha hatari za kuenea kwa virusi hivyo.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni alitangaza hatua mpya za kudhibiti mienendo ya madereva wa malori yanayoingia nchini humo kutoka mataifa jirani baada ya zaidi ya madereva 20 kupatikana na ugonjwa wa Covid-19.

Rais Yoweri Museveni alibaini kwamba madereva hao ni chanzo cha wasiwasi kwa Uganda na ukanda mzima.

Uganda, ambayo imerekodi jumla ya visa 160 baada ya wagonjwa wapya kuthibitishwa, imefanya maelfu ya vipimo kwa madereva wa malori, 51 kati yao, hususan Wakenya na Watanzania, walikutwa na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

Nchi jirani ya Rwanda imebaini kwamba kwa muda wa wiki tatu idadi ya visa nchini humo imeongezeka,miongoni mwa madereva wa malori na wasaidizi wao", bila hata hivyo kutaja idadi yao halisi.Kufikia sasa Rwanda ina visa 287 vya maambukizi ya virusi vya Corona na 168 wamepon augonjwa huo.

Kwingineko nchini Kenya, DRC na Sudani Kusini, madereva wa malori pia wamepatikana na virusi vya Corona.

Kenya sasa imewataka madereva wa malori kufanya vipimo kila baada ya wiki mbili wanapoingia nchini humo na kupewa vithibitisho kwa hilo.

Hivi karibuni Rais wa Uganda Museveni alisema kwamba kupiga marufuku malori kuingia nchini humo itakuwa kama Uganda "imejilipua". Njia ya nchi kavu inasaidia kwa kiasi kikubwa kwa uchumi wa Uganda kama nchi nyingi za ukanda huo.

Sera ya upimaji kwenye vituo vya mpakani nchini Uganda imesababisha mlolongo wa madereva wa malori kwa siku kadhaa.