Coronavirus: Madereva walalamikia kuchelewa kwa matokeo ya vipimo mpakani Kenya na Tanzania
Imechapishwa:
Madereva wa malori ya kubeba mizogo eneo la Afrika Mashariki wanalalamikia zoezi la kupima virusi vya Corona maeneo ya mipakani wakidai linachukua muda mrefu kutoa matokeo ya vipimo.
Kwenye eneo la mpakani kati ya Kenya na Tanzania, eneo la Lunga-Lunga kunamsongamano mkubwa wa malori, madereva wakiarifu kuwa wamesubiri kwa muda mrefu kapata matokeo ya vipimo vya ugonjwa wa Corona ili kuendelea na safari.
“Mimi naitwa kamau Joseph nilipima hapa tarehe 13 nikaambiwa matokeo ni baada ya masaa 48, sasa kila siku naenda pale na bado mpaka leo hayajapatikana”.
“Natoka Tanzania naelekea Lunga-Lunga Perani, leo ni siku ya 4 nasubiri majibu hapa, sasa hatujui kinachoendelea ni kitu gani mpaka saa hizi, twasubiri matokeo ya Kenya kama turudi Tanzania kama tuendelee na safari, “ amesema dereva mwengine.
“Wakenya kama wameeka mikakati yao inabidi mfuate masharti yao ,mwenye ambae anapenda kupima na anapenda kazi yake nendeni mkapime, mwenye hataki abaki, “ amesema Suleiman Chehe, afisa wa Forodha mpakani Lunga-Lunga ambaye anahusika na maswala ya afya.
Serikali kupitia kamishna wa Kaunti ya Kwale, Kusini mwa Pwani ya Karuku Ngumo anasema wanajitahidi kutatua tatizo hilo mpakani ili kupunguza msongamno wa malori.
Ripoti ya Joseph Jira, mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya RFI