Uamuzi wa Mahakama ya Rufaa ya Paris kuhusu kesi ya Kabuga Felicien kujulikana
Imechapishwa:
Majaji kutoka kitengo cha Mahakama ya Rufaa ya jijini Paris nchini Ufaransa hii leo watakutana kuamua iwapo kuna uwezekano wa kuihamishia kesi inayomkabili mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda, Felicien Kabuga katika Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa Rwanda (ICTR) au la.
Wiki iliyopita, mawakili wa mtuhumiwa huyo wa mauaji ya kimbari ya Rwanda yaliyofanyika mwaka wa 1994, Felicien Kabuga walipewa siku 8 kuandaa utetezi wao na kuweka bayana mkakati wao kuhusu mahali wangetamani kesi ya mteja wao isikilizwe.
Jumatano hii waendesha mashitaka kutoka kitengo cha Mahakama ya Rufaa ya jijini Paris watakutana kuamua iwapo mahakama hiyo itamkabidhi Kabuga kwa Mahakama maalum ya Kimataifa ambayo ilichukua nafasi ya ile iliyokuwa inashughulikia kesi za mauaji ya Kimbari nchini Rwanda iliyokuwa mjini Arusha nchini Tanzania au la.
Baadhi ya mawakili wake Kabuga wamekuwa wakipendekeza apelekwe katika mojawapo ya vizuizi vya Umoja wa Mataifa na kesi yake iendeshwe huko.
Mtuhumiwa huyo wa mauaji ya kimbari ya nchini Rwanda mwenye umri wa miaka 84 alikamatwa nchini Ufaransa wiki mbili zilizopita. Alikuwa mafichoni kwa muda wa miaka 26 kabla ya kukamatwa, anatuhumiwa kufadhili mauaji ya kimbari ya Rwanda yaliyoangamiza maisha ya watu zaidi ya 800,000 mnamo mwaka wa 1994.