RWANDA-UFARANSA-ICC-KABUGA-HAKI

Mauaji ya Kimbari Rwanda: Mahakama ya Rufaa ya Paris yafutilia mbali ombi la kuachiliwa kwa Félicien Kabuga

Félicien Kabuga, anayeshtulmiwa kuwa mfadhili mkuu wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, hapa akioneshwa kwa katuni akiwa mahakamani, Mei 20, 2020.
Félicien Kabuga, anayeshtulmiwa kuwa mfadhili mkuu wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, hapa akioneshwa kwa katuni akiwa mahakamani, Mei 20, 2020. Benoit PEYRUCQ / AFP

Mahakama ya Rufaa ya jijini Paris nchini Ufaransa imetupilia mbali ombi la kuachiliwa kwa dhamana kwa Félicien Kabuga, anayedaiwa kuwa mfadhili wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda.

Matangazo ya kibiashara

Félicien Kabuga, mshukiwa mkuu wa mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994, ameiambia Mahakama jijini Paris nchini Ufaransa kuwa mashtaka dhidi yake ni uongo.

Kabuga mwenye umri wa miaka 87, aliyekamatwa mwezi huu nchini Ufaransa anashtumiwa kuwa mfadhili mkuu wa mauaji hayo yaliyosababisha vifo vya watu 800,000 wengi wakiwa Watutsi.

Majaji nchini Ufaransa wanatathmini iwapo afunguliwe mashataka nchini humo au ahamishwe kwenye Mahakama nyingine.

Mawakili wa Félicien Kabuga wamesema umri wake wa miaka 87, pamoja na hali yake ya afya vinamruhusu aachiliwe kwa dhamana. "Kwa sasa hawezi kufanya jambo lolote alilokuwa akifanya kila siku peke yake katika maisha yake ya hapo awali," mwanasheria wake Wakili Laurent Bayon amebaini mbele ya mteja wake, ambaye anatumia kiti cha magurudumu, akihakikisha kwamba hakuwa na nia wala uwezo wa kukwepa vyombo vya sheria na hata kufikia hatari ya kulinganishwa na washtakiwa wengine maarufu kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu.

"Hajawahi kuwekwa katika kifungo cha nyumbani, isipokuwa baada ya kukiuka utaratibu wa sheria za mahakama,"Wakili Bayon amesema, huku akipendekeza mteja wake - badala ya kuwekwa gerezani - apewe kifungo cha nyumbani kwa mtu wa familia yake.

Hoja hizo zimefutiliwa mbali na mahakama ambayo imeunga mkono ombi la upande wa mashtaka, ikionyesha hatari ya mshtumiwa kutoroka, baada ya zaidi ya miaka 20 kuwa mafichoni.