BURUNDI-MAFURIKO-USALAMA

Raia wengi wa Gatumba wasalia bila makazi kufutia mafuriko

Mvua inayonyesha imesababisha Ziwa Tanganyika kujaa na kusababisha mafuriko katika maeneo yaliyo pembezoni ya ziwa hilo, ikiwa ni pamoja na mtaa wa Gatumba.le 12 mai 2010.
Mvua inayonyesha imesababisha Ziwa Tanganyika kujaa na kusababisha mafuriko katika maeneo yaliyo pembezoni ya ziwa hilo, ikiwa ni pamoja na mtaa wa Gatumba.le 12 mai 2010. ROBERTO SCHMIDT / AFP

Kiwango cha maji katika Ziwa Tanganyika kimeongezeka na kusababisha mafuriko katika eneo la Gatumba Magharibi mwa jiji la Bujumbura nchini Burundi na kuacha maelfu ya familia bila makazi baada ya nyumba zao kusombwa na maji.

Matangazo ya kibiashara

Wakazi wa mji wa Gatumba wanaendelea kukabiliwa na hali ngumu baada ya wengi wao kubomokewa na nyumba kutokana na mafuriko yanayosababishwa na Ziwa Tangayika baada ya mvua kunyesha.

“Hapa ni Gatumba, mnajionea wenyewe hali ilivyo, huu ni ule mji uliokuwa na makazi ya watu lakini maji yamegeuza eneo hili kuwa bahari,” amesema mkazi mmoja.

Waakazi wa mtaa wa Gatumba wamelazimika kutumia mitumbwi, katika eneo ambalo kwa sasa limejaa maji, halipitiki, wengi wamepoteza makazi yao.

“Hapa nyumba zote zimebomoka na vitu vyote kusombwa na maji, tumebaki mikono mitupu,” mkaazi mwingine amesema.

Unapotumia helikopta, unajionea athari za kujaa kwa Ziwa Tanganyika zinashuhudiwa umbali wa Kilomita mbili, na makaazi yaliyojaa maji yanaonekana ukitumia ukiwa upande wa Uvira, Kalemie nchini DRC na Kigoma nchini Tanzania.

“ Kuhusu hali ya kiwango cha maji kuongezeka katika Ziwa Tanganyika, ni hali ambayo imewahi kushuhudiwa mwaka 1964 na ni wazi kuwa, kuna uhusiano wa kiwango cha mvua inayonyesha na kusababisha ongezeko hili. Na ukiangalia kiwango cha mvua kilichonyesha kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, na kama ilivyotekea miaka ya 1962, 1963 na 1964 na hii inaonekana wazi kuwa hali ni ile ile, “ amesema Bernard Sindaihebura ni mtalaam wa masuala ya mazingira kutoka Burundi.

Maelfu ya watu wamesalia wakimbizi baada ya makaazi yao kusombwa maji na hakuna mssada wowote waliopata kutoka kwa viongozi wa serikali.

Mara ya mwisho kwa wakazi wa eneo hilo kushuhudia janga hili ilikuwa ni mwaka 1963.