TANZANIA-CORONA-ELIMU-AFYA

Wanafunzi na wazazi wakaribisha hatua ya kuanza tena kwa vyuo Tanzania

Rais wa Tanzania, John Magufuli ametangaza kuwa vyuo vikuu nchini humo vitafungufuliwa Juni Mosi, na kuruhusu pia shughuli zote za michezo nazo ziendelee kama kawaida.
Rais wa Tanzania, John Magufuli ametangaza kuwa vyuo vikuu nchini humo vitafungufuliwa Juni Mosi, na kuruhusu pia shughuli zote za michezo nazo ziendelee kama kawaida. REUTERS/Sadi Said

Wanafunzi wa Elimu ya juu pamoja na wa kidato cha sita nchini Tanzania wameanza muhula mpya wa masomo baada ya serikali kusitisha masomo kwa miezi mitatu nchini humo ili kujihadhari na mlipuko wa Ugonjwa wa Covid-19.

Matangazo ya kibiashara

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nchini humo ni Miongoni mwa vyuo vilivyofunguliwa juma hili.

Hatua hii inachukuliwa baada ya rais wa nchi hii John Pombe Magufuli kuvitaka vyuo kuanza kufunguliwa ili wanafunzi wahitimishe muhula wa masomo, wakati serikali ikiendelea kufuatilia mwenendo wa ugonjwa Covid-19..

Kaimu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayeshughulikia elimu, Profesa Bonaventure Rutinwa, amesema wamechukuwa tahadhari zote muhimu ili kuepuka maambukizi ikiwa ni pamoja na wahadhiri kuwaongeza saa za ufundishaji kutoka saa tatu za kawaida mpaka saa nne kwa kipindi kimoja kwa siku.

“Maana yake kama wewe tumekupatia saa nne una uhuru wa kusema saa ya kwanza watakuja, nusu saa ya pili watakuja hawa, na bado wote wakatimiza saa, tumewapa uhuru wa kuhakikisha kwamba unakuwa na wanafunzi unaoweza kuwamudu, “ amesema Profesa Bonaventure Rutinwa.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliozungumza na idhaa hii wamesema wamejipanga ili wahakikishe wamemaliza muhula wa masomo.

“Tumeshajipanga kiukweli kupambana kusoma kwa bidii ili tumalize, “ amesema mmoja wa wanafunzi hao.

“Muhula wa masomo umefupishwa lazima tuendane na kasi iliyopangwa na chuo, Mwanafunzi mwengine.

Tayari Naibu waziri wa Elimu nchini Tanzania, Tate Ole-Nasha, amevitaka vyuo vya elimu ya juu katika muhula huu kuhakikisha vinatoa elimu kwa kuzingatia ubora.

Wanafunzi sasa wa vyuo vya elimu ya juu nchini Tanzania wanalazimika kusoma kwa majuma 12 na si kumi na manane kama ilivyo kawaida ili kuhitimisha muhula huu wa masomo.